Audio & Video

Kampuni ya Acacia yagharamia matibabu kwa wahanga wa matukio ya moto

on

Baadhi ya watoto na wazazi wakiwa katika hospitali ya mkoa Mwanza, Sekou Toure wakisubiri huduma ya upasuji majeraha na kurekebishwa viungo vilivyoshikana baada ya kupata ajali mbalimbali ikiwemo moto.

Judith Ferdinand, BMG

Wahanga 55 wa matukio ya ajali ikiwemo kuungua kwa moto wameanza kupata huduma ya upasuaji wa makovu pamoja na kurekebisha viungo vya miili yao vilivyoshikana kutokana na matukio hayo, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwanza Sekou Toure.

Huduma hiyo inatolewa kwa wahanga hao wakiwemo watoto kutoka maeneo jirani yanayozunguka migodi ya kampuni ya Acacia ambayo ni North Mara, Bulyanhulu pamoja na Buzwagi.

Akizungumza na wanahabari, Afisa Mahusiano kampuni ya Acacia, Christina Deus alisema wahanga hao wamekuwa wakipata changamoto ya kutengwa katika jamii baada ya kupata majeraha ya moto, uji na chai hivyo huduma hiyo itawasaidia kuimarisha hali zao na kuendelea na shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Alisema huduma hiyo inatolewa na kampuni ya Acacia kwa kushirikiana na Hospitali ya Sekou Toure pamoja na Madaktari kutoka taasisi ya Rafiki Surgical Mission ya nchini Australia na kwamba huduma hiyo inagharimu zaidi ya shilingi Milioni 79.

Deus alisema huduma hiyo ni muhimu kwa wahanga hao kutokana na wengi wao kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu hivyo alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kujitokeza ili kupata matibabu bure.

Naye Mganga Mfawidhi Hospitali ya Sekou Toure, Dkt. Bahati Msaki alisema kuna kambi maalum ya siku kumi kuanzia Oktoba 15 hadi 24 mwaka huu hospitalini hapo kwa ajili ya watu walioungua na moto, maji, uji na chai ambao walitibiwa lakini makovu katika miili yao hayakuisha pamoja na baadhi ya viungo kama miguu kushikana hivyo wananchi wajitokeze kupata bure huduma hiyo ya upasuaji kuondoa makovu hayo pamoja na kutenganishwa viungo vilivyoshikana.

“Jumla ya madaktari bingwa saba wamejipanga kutoa huduma hii ya upasuaji wa makovu ya moto na viungo vilivyoshikana ambapo watatu wanatoka Australia, watatu wengine hapa Sekou Toure na mmoja anatoka Hospitali ya Taifa Muhimbili”. Alibainisha Dkt. Msaki.

Wazazi ambao watoto wao wamefika katika Hospitali ya Sekou Toure walitoa shukurani zao kwa kampuni ya Acacia kwa kuwasaidia kupata huduma hiyo bure.

“Baada ya mtoto wangu kuungua alipatiwa matibabu lakini makovu hayakuisha ambapo nilishindwa kugharamia matibabu zaidi hivyo nimefarijika Acacia kutusaidia gharama za matibabu haya”. Alisema Geofrey Nayinda, mkazi wa Kakola mkoani Shinyanga.

Tazama BMG Online TV hapa chini

Recommended for you