Habari Picha

Askari polisi watakiwa kuwa Makini

on

BMG Habari-Pamoja Daima

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Naibu Kamishina wa polisi Ahmed Msangi amewataka askari polisi kuepuka tabia ya kuwabambikizia wananchi kesi, rushwa pamoja na kufanya kazi kwa ubabaishaji.

Amewataka kufanya kazi kwa bidii, utii, nidhamu na maadili kama ambavyo jeshi la polisi nchini linaelekeza.

Kamanda Msangi aliyasema hayo mwishoni mwa mwezi uliopita (Februari 28, 2018) alipokutana na askari wa wilaya ya sengerema ikiwa ni mwendelezo wa ukaguzi anaoufanya kwa askari na vikosi vyote mkoani Mwanza.

“Mfano kesi ya madai inabadilishwa kuwa kesi ya jinai jambo ambalo linanyima haki wananchi na kuchafua sifa nzuri ya jeshi la polisi. Hivyo ubabaishaji wa aina hii uepukwe na yeyote atakaye bainika anafanya hivyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake”. Alisisitiza Kamanda Msangi kwa askari wenye tabia hiyo ikiwa wapo.

Kamanda Msangi akizungumza na askari wilayani Sengerema.

Aidha Kamanda Msangi aliwataka askari wa vitengo kusimama vyema katika nafasi zao ambapo alisema kila askari akiwa vizuri katika utendaji kazi hakutakuwa na malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi hivyo ni jukumu la kila askari kuhakikisha dhamana aliyopewa na serikali ya kulinda wananchi pamoja na mali zao anaisimamia vizuri bila ubabaishaji wa aina yoyote.

Aliwataka askari kuwa na utaratibu mzuri wa upokeaji, utunzaji na uondoshaji wa vielelezo katika vituo vya polisi kwani katika baadhi ya vituo vya polisi kuna tatizo la utunzaji wa vielelezo, hivyo hataki kuona tatizo hilo linaendelea kuwepo.

“Kwa upande wa upelelezi kumekuwa na tatizo la kuchelewesha upelelezi wa kesi nyingi jambo ambalo linawanyima wananchi haki, hivyo Mkuu wa Upelelezi Wilayani shughulikia suala hilo mapema ili lisiwepo na hakikisha haki inapatikana haraka bila uonevu wa aina yoyote”. Msangi.

Recommended for you