Audio & Video

Benki ya CRDB yasaidia kuboresha huduma za afya na ulinzi Jijini Mwanza

on

Judith Ferdinand, BMG

Benki ya CRDB imetoa msaada wa shilingi Milioni 240 katika hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza ili kuunga mkono juhudi za ukarabati na upanuzi wa jengo la huduma za wagonjwa wa dharura (Emergency Medicine Department) katika hospitali hiyo.

Akizungumza jana kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo nchini, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Uendeshaji na Huduma kwa Wateja Esther Kitoka, alisema benki ya CRDB inaunga mkono juhudi za ukarabati huo kwani utasaidia hospitali hiyo kupokea wagonjwa wengi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuwahudumia kwa wakati mmoja.

Bi.Kitoka alisema alisema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya banki hiyo inayohimiza kuchangia huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo sekta ya afya.

Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Rufaa Bugando Dkt.Abel Makubi alisema licha ya unyeti wa idara hiyo bado inakabiliwa na uhaba wa madaktari hivyo ni vyema serikali ikaajiri madaktari zaidi kwani idadi ya wagonjwa imeongezeka kutoka 50 hadi kufikia 100 kwa siku.

Dkt.Makubi alisema juhudi za hospitali hiyo ni kuhakikisha kitengo hicho kinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa ambapo kupitia mapato ya ndani inaajiri madaktari wa muda hadi serikali itakapoajiri madaktari wa kudumu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi Hospitali ya Bungando, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Mhashamu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi aliishukuru benki ya CRDB kwa msaada huo akisema imeonyesha mfano bora kwamba mbali na kufanya biashara pia inatoa huduma katika jamii.

Katika hatua nyingine benki ya CRDB ilikabidhi msaada wa pikipiki tatu aina ya Boxer zenye thamani ya shilingi milioni 10 pamoja na usajili kwa jeshi la polisi mkoani Mwanza ili kuunga mkono juhudi za jeshi hilo katika kuimarisha hali ya ulinzi na usalama.

Katika makabidhiano hayo, Kitoka alisema benki ya CRDB inatambua umuhimu na mchango wa jeshi la polisi hivyo msaada huo utasaidia kutatua changamoto ya usafiri kwa askari wakati wakitimiza majukumu yao.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi aliipongeza benki ya CRDB kwa kutambua umuhimu wa jeshi hilo na kwamba msaada huo utasaidia kuimarisha shughuli za jeshi hilo.

Thamani halisi ya msaada uliotolewa na benki ya CRDB katika hospitali ya Rufaa Bugando na jeshi la polisi mkoani Mwanza ni shilingi Milioni 250.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Uendeshaji na Huduma kwa Wateja Esther Kitoka, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu CRDB kwenye hafla ya kukabidhi msaada wa shilingi milioni 240 katika hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza. 

Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Rufaa Bugando Dkt.Abel Makubi akizungumza kwenye hafla hiyo. 

Mwenyekiti wa Bodi Hospitali ya Bungando, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Mhashamu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi akitoa salamu za shukurani katika hafla hiyo.

Makabidhiano ya hundi ya mfano ya shilingi milioni 240 kutoka benki ya CRDB ili kusaidia ukarabati na upanuzi wa wodi ya wagonjwa wa dharura katika hospitali ya Rufaa Bugando.

Makabidhiano ya hundi ya shilingi milioni 240 kutoka benki ya CRDB ili kusaidia ukarabati na upanuzi wa wodi ya wagonjwa wa dharura katika hospitali ya Rufaa Bugando.

Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Rufaa Bugando Dkt.Abel Makubi (kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusiana na ukarabati na upanuzi wa wodi ya wagonjwa wa dharura katika hospitali hiyo.

Mkuu idara ya dharura akitoa ufafanuzi kuhusiana na wodi hiyo.

Baadhi ya watumishi wa hospitali ya Rufaa Bugando wakifuatilia hafla hiyo.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi akijaribu kuendesha moja ya pikipiki zilizokabidhiwa na benki ya CRDB kwa jeshi hilo. 

ISOME PIA HABARI HII Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza kuendelea kuboresha mahusiano

Recommended for you