Audio & Video

Shirika la KIVULINI labaini aina mpya ya biashara haramu wilayani Misungwi

on

Mkurugenzi wa shirika la KIVULINI,  Yassin Ally.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Biashara haramu ya baadhi ya wanaume kutoa fedha ili kuwashika wanawake sehemu za siri imetajwa kuibuka atika Halmashauri ya wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za wasichana na wanawake KIVULINI,  Yassin Ally aliyasema hayo jana (SOMA HAPA) kwenye mafunzo kwa viongozi na wadau mbalimbali wanaosaidia mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, yaliyofanyika wilayani Misungwi.

Alisema vitendo hivyo vimekuwa vikishamiri katika kipindi cha mavuno kama sasa ambapo baadhi ya wanaume hutoweka nyumbani na fedha za mauzo hadi milioni 10 na hurejea nyumbani baada ya kuzitumbua zote kwenye starehe.

“Wanatoa kuanzia elfu kumi ili wawashike wanawake sehemu za siri, matiti, mapaja, makalio ama wao washikwe sehemu zao za siri”. Alisema Ally na kuongeza kwamba vitendo hivyo vimesababisha familia nyingi kuwa maskini na kushindwa kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi, Eliurd Mwaiteleke ambaye pia alikuwa Mkufunzi kwenye mafunzo hayo, alieleza kuanza kwa kampeni maalum ya miezi miwili mfululizo kuanzia wiki ijayo ili kutoa elimu katika jamii hatua itakatosaidia kutokomeza biashara hiyo haramu pamoja na aina nyingine za ukatili wa kijinsia katika Halmashauri hiyo (SOMA HAPA).

Hata hivyo Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Issack Ndassa alisema Halmashauri ya Misungwi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo shirika la KIVULINI imepiga hatua kubwa katika kutokomeza ukatili wa kijinsia ikilinganishwa na Halmashauri nyingine. Mwanza ni miongoni mwa mikoa ambayo kiwango cha ukatili wa kijinsia kiko juu ukiwa na asilimia 60 kwa takwimu za mwaka 2015/16 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Mkurugenzi Halmashauri ya Misungwi, Eliurd Mwaiteleke

PIA SOMA Wanafunzi Misungwi kusaidia Jamii kuondokana na Ukatili

Recommended for you