Audio & Video

CCM wilayani Magu kuhakikisha serikali inatekeleza wajibu wake

on

Judith Ferdinand, BMG

Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Magu mkoani Mwanza kimeahidi kufuatilia na kuhakikisha serikali inaleta fedha za miradi mbalimbali kwa wakati ili kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/20 ya chama hicho.

Hayo yamesemwa na Katibu wa CCM wilayani humo ,Waridi Mngumi katika kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya chama hicho kwa ajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2017.

Mngumi alisema ili kutekeleza ilani na wananchi kupata maendeleo wao kama chama watahakikisha serikali inaleta fedha kwa wakati pamoja na kuzisimamia ili zitumike kwenye miradi iliyokusudiwa.

Alisema kwa mwaka jana, sekta ya afya katika kutoa huduma imefanikiwa kwa asilimia mia japo changamoto imejitokeza katika ujenzi wa zahanati,hivyo aliitaka halmashauri ya wilaya hiyo  kuendelea kutoa elimu kwa umma katika suala zima la umuhimu wa kuchangia miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilayani Magu, Isack Zabron alisema kwa mwaka 2017 miradi uliyotekelezwa kwa asilimia mia ni ujenzi wa kituo cha afya Kahangara,ujenzi wa kisima cha maji kata ya Lubugu.

Zabron alisema mradi mkubwa wa maji  umekamilika kwa asilimia 43 ambao utanufaisha Kata nne ikiwemo Magu Mjini, Itumbili, Isandula na Kandawa pamoja na kufanikiwa kupata shule mbili kwa ajili ya kidato cha tano na sita ambazo ni Kitongo Sima na Magu Sekondari.

Naye Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM wilayani Magu, Edwin Mkangara alisema kazi yao ni kuisukuma na kuisisitiza serikali kuifanya Magu  mpya katika kutekeleza ilani ya chama chao ikiwemo ya kumtua ndoo mwanamke kwa kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa na kila kijiji kinayapata.

Alisema wanatengeneza mahusiano mazuri kati ya wananchi na serikali sambamba na kufanya semina kwa viongozi katika maeneo mbalimbali  namna ya kuhamasisha jamii ijue ni wajibu na kujitolea kuchangia maendeleo.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Magu, Ayoub Bindulle alisema vijana wanawajibika katika kuhakikisha ilani inatekelezwa kwa kuhamasisha wenzao kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo huku wakisisitiza halmashauri kutoa mikopo ya asilimia kumi ya mapato yake kwa vijana, wanawake na walemavu ili waweze kujiinua kiuchumi.

ISOME PIA HABARI HII Kamati ya Siasa yaridhishwa na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo Misungwi 

Recommended for you