Habari Picha

Benki ya CRDB yatakiwa kulipa fedha za Ushirika KCU

on

Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt.Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wadau wa Kahawa wilayani Muleba.

Na Mathias Canal-WK, Muleba-Kagera

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt.Charles Tizeba Jana 12 Julai 2018 ameitaka benki ya CRDB kulipa haraka malipo ya fedha za Ushirika za Chama Kikuu cha Kagera (KCU) kulingana na hatma ya kesi iliyokuwa mahakamani mwaka 2003 ambapo wakulima walikuwa wakikatwa kiasi cha shilingi 10 kwa kila kilo moja ya Kahawa ili kujenga mfuko wa mazao kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 1990 hadi 1993.

Dkt.Tizeba alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wadau wa Kahawa wilayani Muleba ikiwa ni siku ya tatu ya ziara ya kikazi mkoani Kagera iliyoanza Julai 10, 2018 na kuhudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage.

Suala la madai hayo katika mkutano huo liliibuka baada ya baadhi ya wakulima kuonyesha vitabu vya mfuko huo ambapo makato hayo ya shilingi 10 kwa kilo kwa kipindi cha miaka mitatu jinsi ambavyo yalikuwa yakifanyika.

Madai ya wakulima hao yamekuwa yakilalamikiwa kwa kipindi kirefu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa imani ya wakulima kwa chama kikuu cha ushirika Kagera (KCU). Chanzo cha kesi hiyo ni baada ya Benki ya CRDB kuzuia fedha za malipo yaliyotokana na mauzo ya Kahawa ili kulipia deni la msimu wa mwaka 1997/1998.

Hukumu ya kesi iliyotolewa tarehe Octoba 28, 2009 na mfuko wa Mazao wa wakulima Mkoani Kagera kupewa tahfifu ulizoomba ambapo tangu wakati huo benki ya CRDB iliweza kulipa fedha za mfuko ilizochukua kiasi cha shilingi milioni 525 na fedha zilizobaki bado hazijalipwa kwa kisingizio cha kuwa na nia ya kukata rufaa ambayo bado haijakatwa ambapo hata hivyo hawawezi kukata rufaa kutokana na muda kuwa umepita.

Dkt.Tizeba alisema kuwa jumla ya madai hayo sambamba na riba ni shilingi bilioni sita za kitanzania huku akisisitiza kuwa benki hiyo ya CRDB inapaswa kuwa mfano wa benki zingine nchini hivyo kushindwa kuwalipa wakulima kwa wakati ni kushindwa kwenda na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli.

Wakati huo huo Waziri Tizeba aliagiza Halmashauri zote nchini zinazolima Kahawa kusimamia ukusanyaji wa zao kupitia vyama vya Msingi (AMCOS) kwani kutokana na usimamizi huo ndio hupata ushuru wa Halmshauri.

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Muleba kusini Mhe. Prof Anna Tibaijuka kabla ya mkutano na wadau wa Kahawa Wilayani Muleba

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage akimakabidhi Mkuu wa Wilaya Mubela Mhe.Richard Ruyango mwongozo wa ujenzi wa viwanda wilayani humo

Wadau wa Kahawa wilayani Muleba wakimsikiliza Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt.Charles Tizeba

Wajumbe waliohudhuria mkutano huo

Recommended for you