Makala

Changamoto ya watoto wanaoishi Mitaani mkoani Mwanza

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Serikali, mashirika binafsi pamoja na wadau mbalimbali wametakiwa kuendelea kutoa elimu ya malezi kwa jamii ili kusaidia kuondokana na uwepo wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ikiwemo mitaani.

Inaelezwa kwamba ongezeko la watoto wanaoishi mitaani ni ukosefu wa huduma muhimu ikiwemo chakula, malazi, wazazi kutowajiba ipasavyo katika malezi pamoja na mifarakano ndoa katika familia.

Hayo yalisemwa na Afisa Ustawi wa Jamii Sekretalieti ya Mkoa wa Mwanza, Wambura Kizito wakati akizungumza na BMG ofisini  kwake.

“Jamii na wazazi wajitahidi kuwa na mikakati kabla ya kuwa na familia ili kujua wanataka watoto wangapi kulingana na hali ya kipato chao kiuchumi na waachane msemo wa kila mtoto na riziki yake kwani umepitwa na wakati”. Alisema Kizito.

Kizito alisema watoto wanapokosa mahitaji muhimu na malezi sahihi kutoka kwa wazazi wao ambao ndio nguzo,  wanakimbilia mitaani kutafuta msaada kutoka kwa wasamaria wema hivyo kujikuta wakiishia kuomba omba.

Pia alisema mwaka jana walibaini jumla ya watoto 56,734 wanaoishi katika mazingira hatarishi mkoani Mwanza, wasichana wakiwa ni 28,911 huku wavulana wakiwa ni 27,823 na kati ya hao kuna wanaoishi mitaani moja kwa moja katika baadhi ya halmashauri ikiwemo wilaya  ya Sengerema  ambapo ina jumla ya watoto 16  wanaoishi mtaani na kati yao waliounganishwa na familia zao  na kurudishwa shule ni 13, wilaya ya Magu ikiwa na watoto 33 na waliorudishwa  nyumbani na kuunganishwa na shule ni 29.

Aliongeza kuwa halmashauri za Jiji la Mwanza na  Ilemela zina jumla ya watoto wanaoishi mitaani  1,421 kati ya hao 343 wameunganishwa na familia zao huku 296 wakirudishwa shuleni na  halmashauri zilizobaki ikiwemo Ukerewe, Kwimba, Misungwi hazikukutwa na changamoto ya kuwa na watoto wa mitaani.

Hata hivyo alisema mikakati ya mkoa ni  kuhakikisha kila halmashauri kupitia Maofisa Ustawi wa Jamii inatoa elimu ya kifamilia na malezi kuanzia ngazi ya Kata pamoja na kubaini changamoto zilizo sababisha mtoto kukimbilia mtaani, kuboresha familia zao kisha kumrudisha nyumbani.

Sambamba na kuongeza kuwa kabla ya kuwarudisha nyumbani wanawaweka kwenye makao ya muda ambapo mkoa wa Mwanza una jumla ya makao 17 ya kulelea watoto wanaoishi  mazingira hatarishi yaliyosajiliwa ambayo yana  jumla ya watoto 669 wakiwamo wasichana 262 na wavulana 407.

Recommended for you