Audio & Video

Benki ya CRDB yasaidia kuboresha huduma za Afya Sekour Toure Jijini Mwanza

on

BMG Habari, Pamoja Daima!

Ukusanyaji wa mapato katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, umeongezeka baada ya hospitali hiyo kuanza kutumia kadi za benki ya CRDB kupokea malipo.

Katibu wa hospitali hilo, Danny Temba ameyasema hayo wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa benki ya CRDB Dr.Charles Kimei, aliyoifanya Jijini Mwanza kutembelea wateja na taasisi mbalimbali zinazotumia huduma za benki hiyo.

Temba amesema kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2016 hadi Januari 2017 hospitali hiyo ilikusanya zaidi ya shilingi Milioni 430 bila kutumia mfumo wa malipo kwa mfumo wa kadi na kwamba malipo hayo yameongezeka kwa kipindi cha mwezi Julai 2017 hadi Januari 2018 hadi kufikia zaidi ya shilingi milioni 530 baada ya mfumo wa kadi kuanza kutumika.

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Dr.Charles Kimei amesema benki hiyo imeboresha zaidi mfumo wa malipo kwa njia ya kadi na kwamba taasisi mbalimbali ikiwemo hospitali zimeanza kunufaika na mfumo huo.

Katika ziara hiyo Dr.Kimei alitembelea pia hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando, Kampuni ya huduma za usafirishaji majini Kamanga Feri pamoja na kampuni ya huduma za meli Marine Services na kubainisha kwamba benki hiyo itaendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kukuza mitaji yao.

Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Marine Services, Eric Hamissi amesema uhusiano baina ya kampuni hiyo na benki ya CRDB, utaimarisha usafiri wa majini kupitia mikopo na hivyo kusaidia ujenzi wa meli mpya na kukarabati meli zilizopo katika Ziwa Victoria na Tanganyika.

Tamati ya ziara hiyo ni Dr.Kimei aliyeambatana viongozi mbalimbali wa benki ya CRDB kukutana na wateja wa benki hiyo Jijini Mwanza, katika hafla fupi ya chakula cha usiku iliyolenga kuwashukuru wateja hao kwa kuendelea kuamini kutumia huduma za benki hiyo.

Mkurugenzi wa benki ya CRDB Dr.Charles Kimei akizungumza jana alipotembelea hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure.

Mganga Mkuu mkoani Mwanza Dr.Leonard Subi akizungumza baada ya kuupokea ugeni kutoka benki ya CRDB ulifika hospitalini hapo kujionea huduma za malipo kwa njia ya kadi zinavyotolewa.

Mwenyekiti wa bodi ya hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure, Christopher Gachuma akitoa neno la shukurani kwa benki ya CRDB kwa ushirikiano wake katika kuboresha huduma za hospitali hiyo. Bonyeza HAPA  kujua zaidi.

Katibu wa hospitali ya Sekour Toure pamoja na watumishi wengine wa hospitali hiyo.

Recommended for you