Audio & Video

DC Misungwi apiga marufuku usafirishaji wa madini

on

Mkuu wa wilaya Misungwi, Mhe. Juma Sweda akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Mkuu wa wilaya Misungwi mkoani Mwanza Juma Sweda amepiga marufuku usafirishaji wa madini ghafi (Cabon) kutoka ndani ya wilaya hiyo kwa ajili ya kwenda kuchenjuliwa katika wilaya nyingine.

Sweda alitoa zuio hilo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya Misungwi, na kuwataka madiwani na watendaji kusimamia kikamilifu utekelezaji wake.

Alisema lengo la kuzuia usafirishaji wa madini ghafi hayo ikiwemo dhahabu na chuma ni kuhakikisha uchenjuaji unafanyikia ndani ya wilaya ya Misungwi ili kuongeza fursa ya ajira kwa wananchi pamoja na ukusanyaji mapato hivyo madini hayo yatasafirishwa baada ya kuongezwa thamani katika eneo (halmashauri) yanapochimbwa kama sheria ya madini inavyoelekeza.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Misungwi, Antony Bahebe alisisitiza madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia vyema suala la ukusanyaji wa mapato ili kufikia lengo la asilimia 100 mwaka 2018/19 kutoka asilimia 80.16 mwaka 2017/18 huku wakihakikisha hakuna upotevu wa mapato ya halmashauri hiyo na kwamba watakaoshindwa kufanya hivyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Kisena Mabuba alisema zuio hilo litasaidia kudhibiti mapato yanayopatikana kutokana na shughuli za uchenjuaji madini hivyo atashirikiana vyema na watendaji wake ili kutekeleza vyema zuio hilo.

Pamoja na kujadili taarifa ya maendeleo ya halmashauri ya Misungwi kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2017/18, pia baraza hilo lilifanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti ambapo diwani wa Kata ya Fella, Paul Kishinda alichaguliwa bila kupingwa kwa kura 34 kushika nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na diwani wa Kata ya Mabuki, Nicodem Ihano.

Mhe. Juma Sweda akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya Misungwi
Mwenyekiti halmashauri ya Misungwi, Antony Bahebe akizungumza kwenye kikao hicho
Mkurugenzi halmashauri ya Misungwi, Mwl. Kisena Mabuba akizungumza kwenye kikao hicho
Makamu Mwenyekiti halmashauri ya Misungwi, Katikista Paul Kishinda (CCM) ambaye alichaguliwa jana akitoa salamu za shukurani kwa kuchaguliwa kwa kishindo
Makamu Mwenyekiti mstaafu halmashauri ya Misungwi, Nicodem Ihano akitoa salamu za shukurani baada ya kustaafu
Zoezi la kuhesabu kura kumpata Makamu Mwenyekiti halmashauri ya Misungwi kwa mwaka 2018/19
Tazama BMG Online Tv hapa chini 

Recommended for you