Audio & Video

“Elimu zaidi inahitajika kupambana na mimba na ndoa za utotoni”- Hakizetu

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Imeelezwa kuwa sheria pekee haiwezi kumaliza changamoto ya mimba na ndoa za utotoni pamoja na ukatili dhidi ya wanawake, badala yake ni kujikita katika kutoa elimu na kubadili fikra na tamaduni hasi kwa jamii.

Hivyo jitihada za dhati zinahitajika katika kubadili mitazamo kuanzia ngazi  ya familia mpaka taifa,kwa mashirika ya utetezi wa haki za binadamu, wanaharakati,serikali na mashirika yanayojihusisha na utetezi  wa haki za  watoto na wanawake kuungana pamoja kuhakikisha changamoto hiyo inamalizika au kupungua.

Hayo yalisemwa jana na Afisa Mradi  wa Shirika  la Hakizetu, Evodius Gervas linalojishughulisha na utetezi wa haki za watoto wa kike na wanawake, katika mafunzo ya siku mbili ya wadau wa shirika hilo, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Maendeleo House jijini Mwanza.

Gervas alisema takwimu zinaonyesha asilimia 85 ya waathirika wa vitendo vya ukatili ni wanawake ambapo wanne kati ya 10 hukumbana na ukatili nchini katika jamii, asilimia 40 ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 na asilimia 21 chini ya miaka 18 wanapata ujauzito ambapo umri huo ni wakuwa shuleni na hivyo kupelekea taifa kuwa na wanawake wengi ambao wameingia kwenye dimbwi la ukosefu wa elimu.

Alisema wazazi wawape watoto wao elimu inayoendana na wakati,na wasidhani wanawafahamu walivyo ili wajitambue,wajifahamu na kujijua na hatimaye kuzuia mimba za utotoni, kwani Tanzania  tunaweka juhudi za kupigana na matokeo ila tunasahau kuanzia visababishi.

“Tatizo la wazazi na jamii wanadhani kuwa wanawafahamu na kuwajua watoto wao,hivyo wanatumia mbinu za zamani katika kumfunza na kumlea mtoto, na wanasahau kuwa sasa ni mabadiliko ya teknolojia,hivyo waendane na wakati katika kutoa elimu na wakubali kujifunza kutoka kwao, kwani kuna mitandao mingi inayotoa elimu mbaya kwa watoto na kupelekea kujiingiza katika masuala ya mapenzi na matokeo yake kupata mimba na ndoa za utotoni katika umri mdogo, alisema Gervas.

Pia alisema wao kama shirika katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii juu ya ukatili,mimba na ndoa za utotoni wamewakutanisha wadau mbalimbali ili wajadili nini cha kufanya pamoja na kuwajengea uwezo wa kujua namna ya kutokomeza ukatili na kupaza sauti.

Hata hivyo alisema, mradi wa Ishi Vizuri Sasa (Living Better Today) umeweza kuwafikia wanaharakati wanafunzi 30 kutoka shule ya Sekondari Ibungiro na Baptist,ambao wamewajengea uwezo wa kujua aina za ukatili  na kuunda vikundi kwa kushirikiana na walimu,ili waweze kuwaelimisha wenzao sambamba na kuvunja ukimya ndani na nje ya shule.

Naye Msimamizi wa Mradi wa Shirika la Hakizetu Bertha John alisema, lengo la mradi wao ni kuona nchi inakuwa haina vitendo vya ukatili, mimba na ndoa za utotoni, na wameanzia wilaya ya Ilemela, na wakishirikiana pamoja  na vyombo vya habari,jamii na wanaharakati kutoa elimu wataweza.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Kujitegemea Paul Bomani alisema kila mmoja ana nafasi yake katika kumlinda mtoto na tatizo nchini tunatunga sheria baada ya kuingia kwenye matatizo huku wezentu wanatunga kabla ya kuingia kwenye matatizo,hivyo hali hiyo inasababisha kuwa na changamoto hiyo.

Bomani alisema, sheria zinazomlinda mtoto na mwanamke ni  Mikataba ya kimataifa, mikataba ya Afrika, mikataba ya Afrika Mashariki,Katiba ya mwaka 1977, sheria ya mtoto no.21 mwaka 2009, sheria ya mikataba ya mwaka 2002, sheria ya ushaihidi,sheria ya Ajira na Mahusiano ya kazi mwaka 2004, sheria ya kanuni za adhabu sura 16 mwaka 2002, sheria ya Elimu na Sheria ya ndoa sura ya 29 mwaka 2002.

Agidius Alloyce ambaye ni polisi Kata Nyamanoro/ Ibungiro alisema katika kuhakikisha tatizo hilo linamalizika kunatakiwa ushirikiano kati ya wazazi, viongozi wa dini na serikali, pia aliwataka wazazi kutoa taarifa endapo binti yao atakuwa amepata mimba katika umri mdogo( akiwa shule) ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Vile vile Mwenyekiti wa  mtaa wa Mkudi Salum Heri aliiomba,serikali kuingiza masuala ya ukatili katika mitahala ya shule ili watoto wawe na uelewa na  watambue tangu wakiwa na umri mdogo.

Recommended for you