Audio & Video

Mafunzo kuhusu “Uwazi wa Uingiaji Mikataba na Uchambuzi wa Taarifa” katika Sekta ya Uziduaji

on

BMG Habari-Pamoja Daima!

Mafunzo kuhusu “Uwazi wa Uingiaji Mikataba na Uchambuzi wa Taarifa” katika sekta ya Uziduaji (madini, mafuta na gesi) yameanza leo jumatatu Februari 26 hadi ijumaa Machi 02,2018 Jijini Dar es salaam. Mafunzo haya yanafanyika Regency Park Hotel Jijini Dar es salaam.

Mafunzo haya yameandaliwa na HakiRasilimali-PWYP yakiwashirikisha washiriki kutoka asasi za kiraia, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kuweza kutambua taarifa na kufanya uchambuzi mahususi kwa ajili ya kufanya uchechemuzi kuhusiana na mikataba ya sekta ya uziduaji.

Mada mbalimbali zitawasilishwa kwenye mafunzo haya, ambapo hii leo washiriki wameangazia juu ya uwazi wa mikataba katika sekta ya uziduaji ambapo wanasema bado hakuna uwazi kwenye mikataba hiyo hali inayosababisha uwajibikaji kukosekana baina ya pande zote mbili (serikali na wawekezaji).

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Linnah Merealle kutoka taasisi ya ADLG ya Jijini Mwanza, anasema ni muhimu kuzingatia suala la uwazi kwenye suala la mikataba na taarifa za utangazaji tenda zinapaswa kupatikana kwa wananchi kabla na baada ya mikataba kusainiwa.

“Hii itasaidia kuwepo kwa uwajibikaji na itapunguza mianya ya rushwa katika mchakto mzima wakuingia mikataba. Pia wananchi wanapaswa kujengewa uwezo ili kutambua umuhimu wa mikataba hii kuwekwa wazi na wapi pa kuipata ili kutambua namna wanavyonufaika na rasilimali zao”. Anasema Merealle.

Lucy Linus kutoka taasisi ya HakiRasilimali, anasema taasisi hiyo imeona ni vyema kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya uziduaji ili kutambua umuhimu wa uwazi na uchambuzi wa taarifa katika sekta ya uziduaji.

Mkufunzi wa mafunzo haya, Joackim Mangilima anasema kuna umuhimu suala la uwazi wa mikataba kuzingatiwa kwani husaidia kuwepo kwa thamani halisi ya matumizi ya fedha, kujenga uaminifu baina ya serikali na wawekezaji na huondoa mianya ya rushwa.

Mkufunzi pia anaeleza uwazi unatakiwa kuwepo katika kila hatua ya mchakato wa uingiaji wa mikataba; Hatua hizo ni mpango, zabuni, mshindi wa zabuni, mkataba, utekelezaji na ufuatiliaji wa mkataba wenyewe.

Soma jumbe mbalimbali hapo chini kutoka HakiRasilimali

Recommended for you