Michezo

JOTO LAPANDA TIMU ZINAZOWANIA KUFUZU ROBO FAINALI NDONDO CUP JIJINI MWANZA

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Timu ya Buzuruga Terminal kutoka wilayani Ilemela, imeshindwa kufuzu kuingia robo fainali (nane bora), katika mashindano ya Ndondo Cup 2017 yanayoendelea kutimua vumbi uwanja wa Nyamagana,licha ya kuichapa Mabatini Star goli 1-0.

Katika mchezo huo, wa lala salama hatua ya makundi, ulizikutanisha timu kutoka kundi B, ambapo Buzuruga Terminal ilifunga goli dakika ya 90 kupitia mshambuliaji wake  Kulu Mashine.

Buzuruga Terminal, imeshindwa kufuzu kutokana na kuzidiwa goli 1 na wapinzani wao Nyegezi Terminal,ambao wameshika nafasi ya pili katika kundi hilo likiongozwa na Mabatini Star.

Mshambuliaji wa timu ya Buzuruga Terminal Maligesi Shaban ndiye aliyeibuka mchezaji bora katika mchezo huo na kujinyakulia kitita cha shilingi 30000 kutoka kwa Hasfu Barber shop.

Shaban alisema, wachezaji wamecheza vizuri japo hawajafanikiwa kufuzu kuingia robo fainali, kutokana na kuzidiwa goli moja na Nyegezi Terminal, hivyo wanajipanga na msimu ujao.

Kwa upande wake Kocha wa Mabatini Star Omary Bakari alisema, anajisikia furaha kufuzu kuingia robo fainali, licha ya kwamba katika mchezo huo hawakufanya vizuri, hivyo wanajipanga kufanya mazoezi ili waweze kufanya vizuri kwa hatua zinazofuatia hatimaye kuibuka mabingwa wa mashindano hayo.

Katika mchezo mwingine uliozikitanisha timu kutoka kundi A,  Iseni Fc na Mnadani zimeshindwa kutunishiana misuli baada ya kutoka sare ya goli 1-1, raundi ya tatu hatua ya makundi.

Iseni Fc ilifunga goli dakika 63 kupitia mshambuliaji Khatibu Abdalah,huku Mnadani Fc wakisawazisha dakika ya 75 kupitia Gama Henry.

Hata hivyo, timu hizo zimefanikiwa kufuzu kuingia  hatua ya robo fainali kwa Mnadani Fc kuongoza katika kundi hilo kwa pointi 7 ikifatiwa na Iseni Fc kwa pointi 5.
Aidha Abeid Athuman kutoka Iseni Fc ndio aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo na kupatiwa 30000.

Recommended for you