Habari Picha

Kampeni ya “Amsha Viwanda” kuzinduliwa Jijini Mwanza

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kesho anatarajia kuzindua kampeni ya “Amsha Viwanda” wilayani Nyamagana jijini hapa.

Kampeni hiyo ambayo itafanyika kwa siku tatu kuanzia Novemba 7 hadi 9, katika ukumbi wa Gand Hall jijini hapa, imelenga  kuwakutanisha wajasiriamali wachakataji wa bidhaa kwa kuwaunganisha na  wadau Wa huduma za kifedha na mamlaka za udhibiti ubora ili waweze kuuza na kusambaza bidhaa zao katika soko la ndani na nje ya nchi.

Hayo yalisemwa jana na  Afisa Mradi wa  Kusaidia na Kuendeleza Wajasiriamali Tanzania (TLED), Elvis Chuwa kutoka Shirika la Voluntary Service Overseas (VSO), ambao ndio waandaaji wa kampeni ya amsha kiwanda wakishirikiana na SIDO, TCCIA, TWCC na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati akizungumza na BMG.

Chuwa alisema,  mradi wa kampeni hiyo kwa awamu ya kwanza utafanyika kwa wilaya nne za mkoa wa Mwanza ikiwemo Nyamagana ambayo ndio wanaanzia, Ilemela, Magu na Kwimba ambapo wamelenga kuwafikia  wajasiriamali 720, huku wakitarajia  250  kupata nenbo ya ubora na 160 ambao ni  wanawake watasajili biashara zao.

“Katika kukamilisha  kampeni hiyo kwenye wilaya nne, tunatarajia wanawake wajasiriamali 160 kusajili bidhaa zao,hii ni kutokana  na wao kukosa masoko ya bidhaa zao kwa vile wengi wao hawajazisajili, hivyo kupitia hivyo tutakua tumesaidia familia na uchumi wa nchi,” alisema Chuwa.

Hata hivyo alisema, kampeni hiyo itawakutanisha wajasiriamali na wadau wa teknolojia ambazo zitawasaidia katika  uzalishaji bidhaa kwa urahisi na bora zinazokubalika,pamoja na TBS  na TFDA kwa ajili ya kujifunza juu ya ubora wa bidhaa.

Aidha alisema, Amsha Viwanda ni  kampeni kwa ajili ya kuwahamasisha wajasiriamali hususani wanawake kwa kuwatangaza na kuunga mkono jitihasa zao kwani wanatambua  jitihada  na changamoto wanazozipata, hivyo wajitokeze kuhudhiria kwani haina gharama yoyote.

Recommended for you