Habari Picha

Alliance yaichabanga GIPCO uwanja wa Nyamagana

on

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Michuano ya Lake Zone Pre-Season Tournament imeendelea hii leo kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza kwa timu ya soka ya Alliance kuifunga timu ya GIPCO ya Mjini Geita magoli 4-0.

Magoli ya timu yote ya timu ya Alliance yametiwa kimiani katika kipindi cha kwanza na wachezaji David Richard (dk 12), Samir Vicent (dk 13), Juhudi Philmon (dk 41) na Martin Kiggi (dk 44).

Kipindi cha pili kilianza kwa timu ya GIPCO kurejea katika hali yake ya mchezo na kuzuia mashambulizi katika lango lake licha ya vijana wa Alliance kumiliki vyema mpira.

Baada ya mchezo huo, kocha wa timu ya GIPCO amesema anatumia mashindano hayo kufanya marekebisho ya kikosi chake kabla ya kuelekea kwenye michezo yake mbalimbali ikiwemo ligi daraja la pili.

Naye kocha msaidizi wa timu ya Alliance, Renatus Shija amekisifu kikosi cha timu ya GIPCO licha ya kupoteza mchezo wa leo akisema si kwamba kikosi cha timu hiyo ni kibovu.

Michuano hiyo inaendelea tena kesho kwa timu ya Singida United kukipiga na timu ya Kagera Sugar ambayo itaingia uwanja ikiwa na kovu la kujeruhiwa na Alliance kwa bao 2-1 katika mchezo wake wa kwanza ambapo GIPCO wao walitoka sare ya bao 2-2 dhidi ya Toto African.

PIA SOMA Michuano ya Lake Zone Pre-Season Tournament kutimua vumbi mwezi huu Jijini Mwanza

Recommended for you