Audio & Video

Timu ya Alliance Girls ilivyoibuka kidedea nyumbani dhidi ya Simba Queens

on

Judith Ferdinand, BMG

Timu ya Alliance Girls ya Jijini Mwanza imeikaribisha Simba Queens ya Jijini Dar es salaam kwa kichapo cha goli 1-0, katika michuano ya Ligi Kuu Wanawake Tanzania inaoendelea nchini.

Mchezo huo ulitimua vumbi  jana kwenye uwanja wa kisasa na mkongwe wa  Nyamagana, ambapo Alliance Girls wakiwa nyumbani waliibuka na ushindi huo na hatimaye kujinyakulia  pointi tatu muhimu ikiwa kama zawadi kwa wanamwanza katika kusherekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka.

Alliance Girls walipata goli dakika ya 18 kipindi cha kwanza kupitia mshambuliaji wake Aisha Juma.

Akizungumzia mchezo huo, Nahodha wa Alliance Girls Enekia Kasonga alisema mchezo na ligi kwa ujumla ni ngumu na timu zote ni  nzuri,hivyo anafurahia ushindi walioupata na hatimaye kujinyakulia pointi tatu wakiwa nyumbani na wanaendelea kujipanga ili waweze kufanya vizuri katika michezo ijayo.

Naye Kocha wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka alisema wamepata pointi tatu na inawezekana wakawa nafasi ya  tatu katika msimamo wa ligi ni kitu cha kujivunia, hivyo wanahitaji  sapoti  kutoka kwa wadau ili waweze kufanya vizuri zaidi.

“Kila mwalimu ana mfumo wake  katika kucheza,ila kikubwa ni sapoti kwani mechi hii ni ya nne bado mechi kama 10, hivyo kuna michezo tunaweza kupoteza kwani hatuwezi kushinda zote na timu itakayopoteza inaipa nafasi nyingine kusonga mbele”. Alisema Chobanka.

Kocha wa timu ya Simba Queens Omary Mbweze alisema walizidiwa kipindi cha kwanza na wapinzani wao wakafungwa goli mapema,pia ratiba ngumu na imewabana sana wanaomba ibadilishwe,hata hivyo wanajipanga ili waweze kufanya vizuri katika michezo ijayo.

Tazama HAPA Michuano ya Compassion Mwanza

Recommended for you