Audio & Video

MAADHIMISHO YA KIFO CHA MWANGOSI YAWATONESHA WANAHABARI

on

BMG Habari, Pamoja Daima!

Waandishi wa habari nchini Tanzania wameendelea kulaani mazingira magumu ya utendaji kazi wanayokumbana nayo ikiwemo kukabiliana na sheria zinazohatarisha uhuru wa habari kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakary Karsan ameyasema hayo hii leo Jijini Mwanza, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya mwanahabari Daud Mwangosi, aliyeuawa na polisi mwaka 2012 akiwa kazini katika Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.

Karsan amesema mbali na waandishi wa habari kukumbana na sheria hatarishi zinazominya uhuru wa habari, pia wanakabiliana na maslahi duni kutokana na serikali kuweka mazingira magumu ya biashara za matangazo kwenye vyombo vya habari wanavyofanyia kazi.

Amesema ni wakati mwafaka sasa waandishi wa habari pamoja na wananchi kwa ujumla kupaza sauti zao kudai mazingira huru kwa wanahabari, akisema serikali inayominya uhuru wa habari ni serikali inayowatesa wananchi wake.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Mwanza (MPC), Osoro Nyawangah amewasihi waandishi wa habari kuiambia serikali kwa uwazi pale inapoenenda kinyume huku akiisihi serikali kuwaacha waandishi wa habari kufanya kazi kwa mjibu wa taratibu za uandishi, akitolea mfano onyo lililotolewa na serikali kwa baadhi ya magazeti baada ya kuripoti suala la bomoa bomoa Jijini Dar es salaam.

Nashon Kenedy ambaye ni mmoja wa waandishi wa habari waliohudhuria maadhimisho hayo amewataka waandishi wenzake nchini kuungana pamoja kama zilivyo taasisi nyingine ili kutetea haki na maslahi yao jambo ambalo litasaidia kuondokana na sheria zinazolalamikiwa kwamba ni kandamizi huku akiwaonya wale wasiotambua umuhimu wa wanahabari kuacha kununua magazeti, kusikiliza redio na kutazama luninga kwani vyombo hivyo ni matokeo ya uwepo wa wanahabari.

Enzi za uhai wake, Daudi Mwangosi alikuwa mwandishi wa habari wa Chanel Ten na pia Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Iringa ambapo aliuawa na polisi Septemba 02,2012 akiwa kazini katika Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa akiripoti habari za mkutano wa kisiasa.

Julai mwaka jana askari huyo mwenye nambari G.2573 Pacificius Cleophace Simon akiwa na miaka 27, alihukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania kutumikia kifungo cha miaka 15 gerezani kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Tazama video na picha hapo chini

Pia Mkurugenzi wa UTPC, Abubakary Karsan amesema Tuzo ya Daudi Mwangosi itatolewa Septemba 17 mwaka huu kwenye Mkutano Mkuu wa UTPC utakaofanyika mkoani Tanga. Mara ya kwanza mwaka 2013 tuzo hiyo ilichukuliwa na Absalom Kibanda ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari 2006 ambapo tangu mwaka huo tuzo hiyo haijawahi kutolewa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa mshindi wake. Baadhi ya sifa za mshindi wa tuzo hiyo ni Mwandishi awe amepigwa, kuumizwa ama kuuawa akiwa kazini ambapo vigezo hivyo vimekuwa changamoto kwa miaka kadhaa katika kumpata mshindi wa tuzo ya Daudi Mwangosi.

Mwenyekiti wa MPC, Osoro Nyawangah akizungumza kwenye maadhimisho hayo

Mwanahabari Pius Rugonzibwa akitoa maoni yake kwenye maadhimisho hayo

 

Mmoja wa wageni washiriki akichangia maoni yake kwenye maadhimisho hayo

Baadhi ya wahudhuriaji wa maadhimisho hayo. Bonyeza BMG Habari, Pamoja Daima kutazama maadhimisho yaliyopita.

Recommended for you