Audio & Video

Maafisa Elimu wanaswa na TAKUKURU Jijini Mwanza

on

BMG Habari, Pamoja Daima!

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Mwanza, imewakamata Maafisa Elimu wawili Jijini Mwanza kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.

Mkuu wa TAKUKURU mkoani Mwanza Ernest Makale amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwl.Mugusi Richard (59) ambaye ni Afisa Elimu Kilimo na Mazingira Jiji la Mwanza pamoja na Mwl.Japhet Mwikwabe ambaye ni Afisa Elimu Taaluma Manispaa ya Ilemela.

Makale amesema maafisa hao wanatuhumiwa kupokea rushwa ya shilingi milioni moja kutoka kwa Bi.Rhobi Kegelo ili wamsaidie kufanya uhamisho wa mtoto wake kutoka shule ya kutwa Jijini Mwanza kwenda shule ya bweni ya Old Moshi mkoani Kilimanajaro jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 15 (1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa No.11/2017.

Inaelezwa kwamba Mwl.Mugusi alipokea fedha hizo kutoka kwa Bi.Rosemary Makenke (57) ambaye ni Afisa Utamaduni Manispaa ya Ilemela aliyetumiwa kupitia simu yake ya mkononi, ingawa watuhumiwa hao wamekana tuhuma hizo mbele ya vyombo vya habari ambapo uchunguzi umekamilika kwa ajili ya kufikishwa mahakamani kujibu mashataka yanayowakabili.

Matukio ya baadhi ya watumishi na viongozi mbalimbali kuomba na kupokea rushwa Jijini Mwanza yameendelea kujirudia ambapo TAKUKURU inawahimiza wananchi kuwafichua viongozi wa aina hiyo kwani ni kosa kisheria kuomba, kupokea na kutoa rushwa.

Bonyeza BMG Habari, Pamoja Daima kutazama wengine waliokamatwa na TAKUKURU.