Audio & Video

Mkurugenzi Misungwi awapiga msasa Watendaji na Viongozi zaidi ya 300

on

Na George Bnagi0GB Pazzo, BMG

Halmshauri ya wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Watendaji na Viongozi mbalimbali zaidi ya 300 ili waweze kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Eliurd Mwaiteleke ambaye alikuwa Mkufunzi kwenye mafunzo hayo yaliyojumuisha wakuu wa idara, maafisa maendeleo ya jamii, watendaji wa kata na vijiji, wenyeviti wa vijiji, madiwani, mahakama, polisi, viongozi wa dini pamoja na sungusungu aliwataka washiriki kuitumia vyema elimu waliyoipata ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Mafunzo hayo yalifanyika kwa siku mbili kuanzia Juni 28, 2018 katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Misungwi kwa ushirikiano na shirika la kutetea haki za wasichana na wanawake KIVULINI ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kitaifa wa kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia.

Katika mafunzo hayo, Mwaiteleke alitangaza kuanza kwa kampeni maalum ya miezi miwili mfululizo kuanzia wiki ijayo ili kutoa elimu kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia na namna ya kuondokana na vitendo hivyo ikiwemo vipigo kwa wanawake, mimba za utotoni pamoja na mauaji ya wazee ambapo washiriki kupitia makundi yao walianzaa mpango kazi namna ya kutekeleza kampeni hiyo.

Mkurugenzi wa shirika la KIVULINI, Yassin Ally alisema shirika hilo linatekeleza mradi wa kuhamaisha jamii kuondokana na ukatili wa kijinsia kwa wasichana na wanawake katika Kata 10 wilayani Misungwi ambapo kupitia mradi huo baadhi ya viashira vya ukatili vimeanza kutoweka katika jamii hususani wakati wa mavuno ambapo baadhi ya wanaume walikuwa wakitoweka na fedha za mauzo na kuacha familia zikitaabika.

Diwani wa Kata ya Misasi, Khalid Mbitiaza ambaye alikuwa mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo alisema yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi na kuahidi kuyatumia vyema kutatua migogoro inayohusiana na ukatili wa kijinsia na pia kuhamasisha jamii kuondokana na vitendo hivyo.

Washiriki wa mafunzo hayo yaliyofikia tamati jana wakimsikiliza Mwezeshaji Eliurd Mwaiteleke

Mkurugenzi shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza kwenye mafunzo hayo

Yassin Ally ambaye ni Mkurugenzi shirika la KIVULINI akifafanua jambo kwenye mafunzo hayo yaliyofikia tamati jana

Mshiriki wa mafunzo hayo, Khalid Mbitiaza ambaye pia ni diwani Kata ya Misasi akichangia mada

PIA SOMA Misungwi kuanza kampeni ya kutokomeza ukatili wa kijinsia

Recommended for you