Habari Picha

Mamlaka na Taasisi za Serikali zatakiwa kuwasaidia Wajasiriamali

on

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhandisi Mtemi Msafiri  akizungumza katika ufunguzi wa kampeni ya amsha viwanda wilayani Kwimba.

Judith Ferdinand, Mwanza

Mamlaka na taasisi za serikali zimehimizwa kuwasaidia wajasiriamali kupiga hatua, ili kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa na viwanda.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhandisi Mtemi Msafiri wakati wa akizindua kampeni ya Amsha Viwanda wilayani humo,iliyoandaliwa na Shirika la Voluntary Service Overseas (VSO) kupitia Mradi wake wa  Kusaidia na Kuendeleza Wajasiriamali Tanzania (TLED) wakishirikiana na SIDO,TCCIA, TWCC na ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza.

Mhandisi Msafiri alisema, kampeni ya amsha viwanda ni muhimu katika kuwezesha wananchi kiuchumi,kuendeleza biashara na viwanda vidogo,na imefanyika wakati muafaka ambapo serikali ya awamu ya tano imejipanga kufanya kazi kwa bidii na maarifa,ili kuleta maendeleo ya haraka kupitia viwanda kwa wananchi wa Kwimba na taifa, hivyo mamlaka na taasisi za serikali zinatakiwa kuwasaidia wajasiriamali hao.

Alisema,  idadi ya wajasiriamali wa uchakataji wa bidhaa mbalimbali wanapata changamoto ya masoko ya ndani na nje ya nchi kutokana na bidhaa wanazozalisha kupata ushindani kwa vile zinakua na ubora hafifu,kutokua na uelewa wa matumizi sahihi ya teknolojia,ukosefu wa mtaji,mafunzo na ushauri wa  biashara, sambamba na ufahamu wa namna ya kufikia huduma zinazotolewa na mamlaka ya udhibiti ubora wa  bidhaa.

Pia alisema, ili kufanikisha maendeleo ya biashara na ujasiriamali,kampeni hiyo imelenga kuwaongezea uelewa wafanyabiashara juu ya upatikanaji wa huduma mbalimbali zitakazo wezesha maendeleo ya biashara zao,hivyo aliwaomba washiriki watumie fursa hiyo vizuri.

Kwa upande wake Afisa Mradi wa TLED kupitia shirika la VSO  Elvis Chuwa alisema, kampeni hiyo kwa awamu ya kwanza wameweza kuwafikia wajasiriamali zaidi ya 700 ambayo imefanyika katika wilaya nne ikiwemo Nyamagana, Ilemela, Magu na wanahitimisha Kwimba,ikiwa imelenga kuwakutanisha wajasiriamali na taasisi   za fedha,udhibiti ubora,  teknolojia,kuonyesha ubora wa bidhaa unaohitajika katika soko la ndani na nje ya nchi, kutoa mafunzo ya kuendeleza biashara na kuhamasisha uanzishwaji viwanda.

Chuwa alisema,  mwitikio Wa wajasiriamali  katika wilaya zote ni  mkubwa,hivyo mpaka sasa wameweza kuwaunganisha wajasiriamali 18 na soko la nje kwa kwenda kushiriki maonyesho ya Jua Kali nchi Burundi,huku wakiwafikia 283 ambao wamefanikiwa na kupiga hatua na kuweza  kutoa ajira kwa wengine.

Pia alisema,changamoto inayowakabiri wajasiriamali ni  mtaji ambapo wao wameweza kuwaunganisha na taasisi za kifedha na kuwapa elimu ya kutumi fedha hizo, hivyo aliwaomba kubadili  fikra na mitazamo yao kwa kutumia fursa zilizopo kwa ustawi wa biashara na uchumi.

Naye Meneja wa  SIDO mkoa wa Mwanza Bakari Songwe alisema, wanampango wa kuanzisha viwanda kila wilaya,hivyo baada ya kampeni hiyo wajasiriamali wataendelea kupatiwa mafunzo,ili kuhakikiaha kunakuwa na viwanda vidogo vilivyosajiliwa sambamba na bidhaa zenye ubora na zilizorathimishwa.

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Pendo Malabeja alisema, fursa hiyo ni chachu ya kufanya wajasiriamali wa Kwimba kukimbia na kwenda haraka katika kufikia uchumi na kuleta maendeleo, ikizingatiwa Rais Magufuli anataka kila Mkoa kuwa na viwanda 100,ambapo Mkuu wa  Mkoa John Mongella ameagiza kuanzia desemba mpaka juni 2018,wilaya hiyo iwe na viwanda 10,hivyo wanauwezo wa kufikisha na zaidi hasa kupitia kampeni hiyo itakuwa nafasi ya kutekeleza agizo hilo.

Mmoja wa wajasiriamali kutoka wilayani Kwimba walioshiriki kampeni hiyo Gertruda  Mdungile alisema, ni fursa ya kujiimarisha katika ujasiriamali na kujengewa uwezo wa kitaalamu na kisayansi katika kutumia teknolojia.

Vilevile Afisa Masoko wa TCCIA Mwanza Joshua John alisema, wanashawishi na kutetea wafanyabiashara,wenye viwanda na kilimo kwa serikali, pia wanawakutanisha wajasiriamali na wachakataji wa bidhaa na wanunuzi kwa kuwatafutia fursa za kibiashara kupitia maonyesho sambamba na kutoa mafunzo kwa wenye viwanda kulingana na mahitaji.

Afisa Mradi wa TLED wa Shirika la VSO Elvis Chuwa akizungumza katika uzunduzi huo.

Recommended for you