Habari Picha

Watumiaji wengi wa vipodozi vyenye sumu ni wanawake- TFDA

on

Judith Ferdinand, BMG

Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini TFDA imeendelea kuwatahadharisha wananchi kuepuka matumizi ya vipodozi vyenye viambato sumu huku ikiwahimiza kutoa taarifa pindi waonapo vipodozi vya aina hiyo sokoni.

Fundi sanifu wa dawa kutoka mamlaka hiyo Kanda ya Ziwa, Kapilya Haruni aliyasema hayo jana kwenye Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika kwenye uwanja wa Nyamhongolo Jijini Mwanza.

Aidha aliwahimiza wanawake kujiepusha na vipodozi vilivyopigwa marufuku na mamlaka hiyo vikiwemo Carolight, toplemon na vyenye mercurya huku kibainisha kwamba asilimia kubwa ya wanaotumia vipodozi vyenye sumu ni wanawake jambo ambalo ni hatari kwao.

Alisema TFDA itaendelea kudhibiti vipodozi hivyo kwa kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali hususani kupambana na baadhi ya wafanyabiashara wanaoingiza vipodozi hivyo kwa njia za panya.

Naye  Mkaguzi wa chakula TFDA Kanda ya Ziwa, Deus Mlenga alisema mamlaka hiyo inashirikiana na mamlaka nyingine ikiwemo Shirika la Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutoa elimu kwa wananchi na wajasiriamali kuhusu umuhimu wa kuandaa na kutumia bidhaa zenye ubora ikiwemo kuwa na vifungashio bora katika bidhaa zao hususani za chakula.

Recommended for you