Habari Picha

Wanaohujumu zao la Kahawa waonywa

on

Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt Charles Tizeba akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa zao la Kahawa uliofanyika jana Julai 10, 2018 katika ukumbi wa Isingiro wilayani Kyerwa.

Na Mathias Canal-WK, Kagera

Biashara ya kuuza Kahawa nje ya nchi bila kufuata utaratibu wa kisheria (magendo) imepigwa marufuku hivyo atakayebainika kuendelea na biashara hiyo atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Agizo hilo limehusisha pia zuio la wananchi kuuza Kahawa mbichi ingali bado shambani haijakomaa (Butura) kwani kufanya hivyo ni kudhoofisha na kuzorotesha juhudi za muda mrefu alizotumia mkulima wa kahawa na kumkosesha mapato stahiki.

Marufuku hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba wakati akizungumza na wadau wa zao la Kahawa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isingiro Wilayani Kyerwa.

Waziri Tizeba alisema kuwa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 ambayo ndio mkataba wa wananchi na serikali yao inatoa maelekezo ya kuwezesha upatikanaji wa Masoko ya Mazao ya Kilimo kwa kuviimarisha na kuviwezesha vyama vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ya ndani na nje kwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji, uchambuzi na uenezaji wa taarifa za Masoko na kutoa elimu juu ya uongezaji thamani na biashara.

Alisema serikali itajitahidi kutafuta bei nzuri ya zao la kahawa ndani na nje ya Afrika Mashariki ili wananchi wapate faida na tija ya Kilimo huku akieleza kuwa wakulima wa kahawa kote nchini hawawezi kuona mafanikio ya Kilimo hicho kwa kuendeleza biashara ya magendo sambamba na biashara ya kahawa mbichi ikiwa shambani (Butura).

Alisema kumekuwa na malalamiko mengi kwa wananchi hususani baadhi ya wakulima wa kahawa kuuza zao hilo nje ya nchi kinyume na sheria kwa hoja ya kwamba wanauza bei kubwa kuliko ndani ya nchi hivyo ili kutambua gharama ameahidi kufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirika kutoka Uganda anayeshughulikia mambo ya ushirika ili kujua kama kweli Uganda kuna wanunuzi wenye uwezo wa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kuliko wanunuzi wa Tanzania ili wapewe utaratibu bora wa namna ya kuja Tanzania kununua Kahawa.

Aidha Waziri Tizeba aliagiza wakulima waliouza kiasi kidogo cha kahawa wasilipwe kwa utaratibu wa benki ili kuepusha usumbufu badala yake kwa wale wakulima waliolima hekari nyingi na malipo yao yatahusisha kiasi kikubwa cha fedha walipwe kwa utaratibu wa njia ya benki.

Aliongeza kuwa mafanikio ya kilimo nchini hususani zao la Kahawa ni lazima kuuza kupitia vyama vya msingi vya ushirika ambapo ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM sura ya pili kipengele cha 21 (n) inaeleza jinsi sheria ilivyofanyiwa marekebisho na kuanzisha sheria mpya ambayo imeanzisha tume huru ya ushirika ili kuwa na tija kwa wakulima kwa ajili ya kuwapatia faida kubwa ya  kuuza kupitia ushirika.

Sambamba na hayo pia Waziri wa Kilimo Mhe.Tizeba amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Shadrack Mhagama kukamilisha haraka iwezekanavyo kiwanda cha kukoboa Kahawa cha Omkagando kilichozinduliwa na mwenge wa Uhuru tangu mwaka 2016 kwa gharama za serikali lakini mpaka sasa kimeshindwa kuendekezwa.

Katika ziara hiyo Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage walitembelea na kuzungumza na viongozi wa Chama Cha Msingi cha Karukwanzi.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage akizungumza kwenye mkutano huo

Wadau wa zao la Kahawa wakifatilia kwa makini mkutano

Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Tizeba wakikagua na kuzungumza na viongozi wa Chama Cha Msingi cha Karukwanzi wilayani Kyerwa.

Recommended for you