Audio & Video

Vijana wa UVCCM Magu wakabidhiwa Mashine ili kuanzisha Kilimo cha Umwagiliaji

on

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) anayewakilisha kundi la Vijana Taifa Mhe.Maria Kangoye (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Magu Ayoub Bindulle mashine ya kusukumia maji kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Judith Ferdinand, BMG Habari

Mbunge wa Viti Maalumu kupitia UVCCM, Mhe.Maria Kangoye amekabidhi mashine ya kusukuma maji (Water Pump) kwa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Magu mkoani Mwanza ili kuwasaidia kuimarisha mradi wa kilimo cha umwagiliaji.

Kangoye alitoa mashine hiyo jana wakati wa Baraza la UVCCM wilayani Magu na kuwahimiza vijana kuitunza na kuitumia vyema mashine hiyo ili kuwanufaisha vijana wengine zaidi na kwamba itawasaidia kusonga mbele kimaendeleo ikiwa watajikita ipasavyo kwenye shughuli za kilimo hasa kilimo cha mboga mboga.

Alisema mashine hiyo ina uwezo wa kusukuma maji umbali wa mita 600 hivyo itasaidia umoja huo katika kilimo cha umwagiliaji kwani shamba lao lipo umbali wa mita 200 kutoka kwenye chanzo cha maji.

Pia aliutaka umoja huo kuwa na moyo wa kushiriki katika fursa na shughuli mbalimbali zinazojitokeza na wawe wabunifu kwani wakati ni sasa hivyo wasiogope kutumia fursa zinazowazunguka ili kutimiza ndoto zao.

Aidha alisema vijana ni nguzo ya chama hivyo wawe mfano mzuri wa kuigwa kwa kufanya shughuli za kijamii pamoja na kujiepusha na utumiaji wa dawa za kulevya.

Mbali na kutoa msaada huo wa mashine, pia Mhe.Kangoye aliitembelea familia ya aliyekuwa Mwenyekiti UVCCM tawi la Itumbili wilayani Magu, Majaliwa Said aliyefariki mwezi Februari mwaka huu na kutoa pole kwa wanafamilia.

Mwenyekiti UVCCM wilaya ya Magu, Ayoub Bindulle alisema vijana wilayani humo wanataka kufanya mabadiliko makubwa kiuchumi na kwamba jumuiya hiyo itatumia fursa ya kilimo cha mboga mboga kwani wameisha pata shamba pembezoni mwa mto Simiyu ambapo ni umbali kutoka mtoni ni mita 200.

Bindulle alimshukuru mbunge Kangoye kwa kuwasaidia mashine hiyo na kuahidi kuitunza, kuilinda na kuifanyia kazi ya uzalishaji na baada ya miezi mitatu watamualika kuja kuangalia mradi wa kilimo/ shamba unavyoendelea.

“Vijana hawawezi kupiga hatua bila ya kuwa na uchumi mzuri hivyo sisi kama UVCCM wilaya tumeanza na mradi wa kilimo kwani mashine na maji tunavyo, kazi tulionayo ni kwenda shambani, na tumeanzisha kamati ya uchumi ya jumuiya yetu itakayosimamia shughuli za  kiuchumi hivyo nawaomba wana umoja tufanye kazi kwa kushirikiana ili vijana wengine waje kujifunza kutoka kwetu.” Alisema Bindulle.

Naye Katibu wa CCM wilaya ya Magu, Warid Mngumi alisema vijana wasipuuze pale fursa  zinapojitokeza na wafanye kazi kwa pamoja ili kujenga chama na kwamba viongozi chama kuanzia ngazi mbalimbali ikiwemo Kata watumie fursa zilizo katika maeneo yao na kuanzisha miradi ya uzalishaji.

Recommended for you