Audio & Video

Mbunge Maria Kangoye awawezesha Vijana Nyenzo za Kilimo wilayani Misungwi

on

Kushoto ni mbunge wa Viti Maalumu (CCM) anayewakilisha vijana Taifa, Maria Kangoye akiwakabidhi majembe vijana wa UVCCM Kata ya Buhingo katika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa UVCCM wilayani Misungwi Kamuli Zacharia  na wa pili ni Katibu wa UVCCM Misungwi, Julius Antony.

Judith Ferdinand-BMG Habari

Vijana nchini wametakiwa kuunda na kusajili vikundi vya uzalishaji mali ili kunufaika na mikopo ya asilimia nne inayotolewa na halmashauri kutokana na mapato ya ndani na hivyo kujikwamua kiuchumi.

Itakumbukwa kwamba halmashauri zote nchini hutenga asilimia 10 ya mapate yake ya ndani kwa ajili ya akina mama, vijana pamoja na walemavu ambapo akina mama hupata asilimia nne, vijana asilimia nne pia na walemavu asilimia mbili ambapo fedha hizo hutolewa kama mikopo yenye riba na masharti nafuu.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) anayewakilisha Vijana Taifa, Mhe.Maria Kangoye aliyasema hayo jana alipowatembelea vijana wa Umoja wa Chama cha Mapinduzi  (UVCCM) Kata ya Buhingo iliyopo wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, kusikiliza kero za wananchi pamoja na kukabidhi majembe ya mkono 25 kwa ajili ya kuwahamasisha vijana wa Kata hiyo kujikita katika kilimo na kujiinua kiuchumi.

Kangoye aliwasisitiza vijana kutumia vyema majembe hayo na kuwataka yakazalishe zaidi kwani kilimo kwani kinalipa endapo watawajibika ipasavyo na kuahidi pia kufanyia kazi baadhi ya changamoto walizomueleza.

“Vijana nawaomba mfanye kazi kwa bidii kwani taifa kwa sasa linataka watu wanaochapa kazi na  muipiganie asilimia tano kwa kuhakikisha mnajiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali na kwenda halmashauri kusajili na kujua taratibu za kupata fedha hizo”. Alisema Kangoye.

Pia aliwataka vijana kujifunza kutoka kwa kina mama ambao wamekua mstari wa mbele kuchangamkia fursa za maendele huku pia akiwasihi viongozi kukaa na wananchi ili kujua changamoto zinazowakabili na kuzitatua.

Aidha aliwasihi wazazi kuwasisitiza watoto wao kwenda shule ili baadaye wawakomboe katika maisha maana serikali imetangaza kuwa elimu ni bure na atakayechangishwa fedha au michango yoyote atoe taarifa.

Pia Kangoye alipata fursa ya kuwakabidhi kadi za CCM vijana 15 waliohama kutoka CHADEMA na kujiunga na chama hicho huku 26 wakipatiwa kadi za kujiunga na UVCCM kata hiyo Kata ya Buhingo na kuwapongeza kwa maamuzi ahihi waliyofanya ya kujiunga na chama kinachojali vijana kwa kuwaletea maendeleo.

Kwa upande wake Katibu wa UVCCM Kata ya Buhingo, Julius Anthony alimshukuru mbunge Kangoye kwa kuwapatia majembe hayo na kuwataka vijana hao kuyatunza na kuyafanyia kazi.

Alisema mikakati ya UVCCM Kata hiyo ni kuhakikisha kila Tawi linakua na kikundi cha kilimo na ufugaji wa kuku, kujenga ofisi ya CCM kata na kushawishi vijana kujiunga na umoja huo.

Pia alisema Kata hiyo ina jumla ya wanachama wa UVCCM 378 lakini wenye kadi ni 83 na 295 hawana kadi hivyo aliomba kufikishiwa kadi ili kila mwanachama anayelipia akabidhiwe kadi yake papo hapo.

Naye Mwenyekiti UVCCM Wilaya ya Misungwi, Chanila Mwakyoma aliwasisitiza  vijana wa umoja huo Kata ya Buhingo kusajili kikundi chao na kuanzisha mradi wa kilimo na kwamba wataungwa mkono. Alisema ofisi ya CCM wilaya iko tayari kuchangia ujenzi wa ofisi ya CCM ya Kata Buhingo na kwamba suala la upungufu wa kadi za CCM atalifanyia kazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti UVCCM Mkoa wa Mwanza, Jonas Lufungulo alisema serikali kupitia halmashauri imekuwa ikitenga fedha za vijana kutokana na mapato ya ndani ili kuwasaidia kupata mikopo yenye masharti nafuu hivyo vijana waitumie vyema fursa hiyo kwa kuunda vikundi vya ujasiriamali kwa ajili ya uzalishaji na kuacha kulalamika kwamba hakuna ajira.

Mbunge wa Viti Maalumu CCM anayewakilisha vijana Taifa, Maria Kangoye akizungumza na vijana wa UVCCM Kata ya Buhingo wilayani Misungwi, kabla ya kuwakabidhi majembe kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali.

Baadhi ya wakazi wa Misungwi wakiwemo wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM wakifuatilia kwa ukaribu mkutano huo.

Mbunge wa Viti Maalumu CCM anayewakilisha vijana Taifa, Maria Kangoye na viongozi wengine wa CCM wakisikiliza hoja za vija wa Misungwi pamoja na kuzungumza nao.

Mmoja wa wanachama waliojiunga na CCM kutoka Chadema akikabidhiwa kadi na Mbunge wa Viti Maalumu CCM anayewakilisha vijana Taifa, Maria Kangoye.

Mbunge wa Viti Maalumu CCM anayewakilisha vijana Taifa, Maria Kangoye akiwa kwenye picha ya pamoja na wanachama wapya waliojiunga na CCM katika Kata ya Buhingo wilayani Misungwi.

Mbunge wa Viti Maalumu CCM anayewakilisha vijana Taifa, Maria Kangoye (wa pili kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa UVCCM wilayani Misunwi Chanila Mwakyomba, wakati akizungumza kwenye zoezi la kukabidhi majembe kwa vijana wa UVCCM Kata ya Buhingo wilayani humo. Tazama HAPA chini UVCCM Magu wakikabidhiwa mashine. 

Recommended for you