Habari Picha

Shirika la HakiZetu laanza midahalo ya wazi kupambana na mimba za utotoni

on

Judith Ferdinand, BMG

Mimba za utotoni zimekuwa kikwazo kwa watoto wa kike kushindwa kutimiza ndoto zao, hivyo elimu ya jinsia inatakiwa kutolewa ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Hii itasaidia wasichana kujitambua na kujua namna ya kuepuka na changamoto zinazopelekea  wao kujiingiza kwenye mapenzi wakiwa na umri mdogo na hatimaye kupata mimba za utotoni.

Wito huo ulitolewa jana na Afisa Mradi wa Shirika la Hakizetu, Evodius Gervas linalojishughulisha  na utetezi wa watoto wa kike na wanawake, katika mdahalo wa kutoa elimu kwa mabinti wa mtaa wa Mkudi uliopo kata ya Nyamanoro Manispaa ya Ilemela, uliongozwa na wanaharakati wa  kujitolea ngazi ya jamii wa  shirika hilo.

Gervas alisema ili kuondokana na hali hiyo elimu inatakiwa kutolewa sambamba na kuwapa mifano hai, pia kwa wasichana waliopata fursa ya kuhudhuria mdaharo huo wanajukumu la kuelimisha wenzao.

Alisema kuna haja ya kuelimisha jinsia zote juu ya mimba za utotoni sambamba na kuwataka mabinti kujitambua na kujua nini wanataka kwa kuepeka kujiingiza katika mapenzi wakiwa na umri mdogo kwani mbali na mimba wanaweza kupata magonjwa ya ngono pamoja na ukimwi.

Kwa upande wake Mwanaharakati wa kujitolea ngazi ya jamii wa  shirika hilo, Jamila Moshi alisema wameisha elimisha jamii kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni,hivyo wataongeza bidii ya kuhamasisha kwa kutembelea maeneo tofauti  yenye  mkusanyiko wa watu kwa ajili ya kutoa elimu kama shuleni,kanisani,msikitini na sokoni.

Naye Mwezeshaji kutoka shirika la Haki Zetu, Jesca Godfrey alisema tangu wanaharakati ngazi ya jamii kuanza kazi januari mwaka huu wameweza kuwafikia watu 300 na kuwapatia elimu juu ya mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia.

Godfrey alisema kupitia wanaharakati ngazi ya jamii watasaidia  kupunguza au kumaliza changamoto ya mimba za utotoni, kwa sababu wanatafikia watu wengi na kwa ukaribu.

Mmoja wa wanufaika wa  mdaharo huo Rahma Issack alisema, ameweza kujifunza namna ya kukabiliana na mimba za utotoni, hivyo atatumia elimu aliyoipata kuelimisha ndugu zake  na jamii kwa ujumla na kuondokana na changamoto hiyo pamoja  na kuliomba shirika hilo kuongeza juhudi ili kufikia malengo.

Recommended for you