Audio & Video

MPC: Wanahabari wamejisahau

on

Judith Ferdinand, BMG Habari

Waandishi wa habari mkoani Mwanza wametakiwa kujielekeza katika kutafuta namna ya kuwa na chama cha wafanyakazi wanahabari ili kutetea maslahi yao kama ilivyo kwa sekta nyingine.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Osoro Nyawangah alitoa rai hiyo jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika kimkoa katika ukumbi wa Nyakahoja Jijini Mwanza.

Osoro alisema waandishi wajielekeze na kuhakikisha wanakuwa na umoja ambao utakuwa na nguvu katika kutetea masuala yanayowahusu pamoja na kuzidisha umoja na mshikamano miongoni mwao.

“Waandishi hatuna chama cha wafanyakazi na tumeridhika, kwani waliojiunga katika vyama vya wafanyakazi siyo sahihi maana havijamlenga moja kwa moja hivyo tujikite katika kupata umoja huo, Chama cha Walimu Tanzania na vyama vingine vimekuwa na nguvu kutokana na sisi wanahabari”. Alisema Osoro.

Alisema wanahabari wamekuwa mstari wa mbele kusemea sekta nyingine ila wao wamejisahau kwani anaamini kuwa waandishi ni wasomi na wanafanya kazi za watu wengi kwa kuhoji walimu, serikali, polisi na kila sekta.

Naye Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella alisema serikali inatambua umuhimu wa wanahabari katika kuchangia maendeleo hivyo aliwaomba washirikiane hasa kwa mambo yanayohusu taaluma na kwamba yuko tayari kuwajengea uwezo.

Katibu Tawala wilaya ya Nyamagana, Yonas Alfred alisema serikali inatambua mchango wa wanahabari na hivyo kuomba ushirikiano baina ya pande zote na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma ili kufikia maendeleo ya mkoa na kuibua changamoto zinazoikabili jamii.

Hata hivyo Katibu wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) mkoa wa Mwanza, Boniphace Nkobe alisema waandishi wa habari wengi wanajikita mjini hivyo ni vyema wakaenda na Vijiji ambako kuna changamoto nyingi huku akishauri wanahabari kutenga siku maalumu kwa ajili ya kupeana semina ya kujua wapi wamefanya vizuri  ama vibaya katika kazi zao.

Bonyeza HAPA kwa taarifa zaidi. 

Recommended for you