Habari Picha

Mabaraza ya wafanyakazi Mwanza yatakiwa kusimama imara

on

Judith Ferdinand, BMG Habari

Waajiri na wasimamizi wa sehemu za kazi wametakiwa kuhakikisha mabaraza ya wafanyakazi yanafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) 2018 yaliyofanyika kimkoa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mongella alisema anataka kufikia Mei Mosi ya mwaka ujao asikie mabaraza ya wafanyakazi yanafanyika kwa asilimia 100 kwa mujibu wa taratibu ambapo yanatakiwa kufanyika si chini ya mara mbili.

Alisema kufanya vikao vya baraza la wafanyakazi ni muhimu kwani  ni sehemu ya mwaajiri na waajiriwa kukutana na kujadili changamoto wanazokabiliana nazo kwa maendeleo ya taasisi au kampuni.

“Mkoa na halmashauri haviwezi kuvumilia kwa kutofanyika vikao vya baraza la wafanyakazi, hivyo nawaomba waajiri na wasimamizi wa sehemu za  kazi kuhakikisha yanafanyika mara mbili  kwa kufuata taratibu na vyombo husika vihusishwe ili kutatua changamoto zetu”. Alisema Mongella.

Pia alisema nia ya serikali  ni kufanya wafanyakazi kuwa na amani ili walete tija katika kazi zao hivyo aliviomba vyama vya wafanyakazi ishirikiane nayo, katika kutatua changamoto zinazokabili kundi hilo.

“Ajenda zetu za maendeleo haziwezi kutimia bila ya juhudi za wafanyakazi, hivyo serikali inatambua umuhimu na mkoa utaendelea kushirikiana na Shirikisho la Vyama Tanzania (TUCTA) mkoa wa Mwanza katika kutatua changamoto zao,” alisema Mongella.

Hata hivyo aliwapongeza waajiri na wasimamizi katika maeneo ya kazi waliofuata maagizo ya zawadi kwa wafanyakazi bora, ikiwa ni njia ya kuleta ufanisi na morali ya kufanya kazi kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Katibu wa TUCTA Zebedayo Athuman  alisema, mabaraza ya wafanyakazi yanafanyika kwa asilimia 80 hivyo wanataka yafanyike mara mbili kama inavyotakiwa pamoja na zawadi za wafanyakazi bora ziwe zinatolewa papo kwa papo katika maadhimisho.

Athuman alisema, wapo pamoja na Mkuu wa Mkoa katika kutatua changamoto za wafanyakazi  kwa ustawi wa taifa.

Recommended for you