Audio & Video

Mfuko wa NHIF watoa onyo kwa wanaoazimana kadi za matibabu

on

Judith Ferdinand, BMG

Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wameonywa kuacha kufanya  udanganyifu wa matumizi ya kadi moja kwa zaidi ya mtu mmoja kwani ni kinyume cha sheria.

Onyo hilo limetolewa na Meneja wa mfuko huo mkoani Mwanza, Jarlath Mushashu wakati akizungumza kwenye kikao cha washauri na viongonzi wa wanafunzi kilichofanyika jana jijini Mwanza.

Alisema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wanachuo pamoja na wananchi ambao ni wanachama wa mfuko huo kwa mhusika kumpatia mtu mwingine kadi ya bima ili akapatiwe matibabu.

“Kitendo cha mwanachama kumpatia kadi mtu mwingine ili apatiwe matibabu ni kinyume cha sheria kwani ni kuhujumu mfuko na kuwakosesha ambao ni wanachama kupata fursa ya matibabu hivyo wenye tabia hiyo waache na atakayebainika sheria itafuata mkondo wake”. Alisema Mushashu.

Mushashu alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanachuo na wananchi kwa ujumla kujiunga na bima ya afya ambayo humsaidia mwanachama kuwa na uhakika wa matibabu wakati wote bila kujali  hali ya kifedha na kiafya aliyonayo kwa wakati huo.

Pia alisema kupitia bima, mwanafunzi anapata matibabu ambayo ni gharama pale anapougua hata akiwa nje ya chuo ama mkoa mwingine katika kipindi cha likizo na bila kujali hali ya kiafya aliyonayo mwanachama.

Naye  Afisa Matekelezo kutoka NHIF Mkoa Mwanza, Ricky Jonathan  alisema changamoto iliyopo ni wanachuo kutokuwa na elimu ya uelewa kuhusu masuala ya mbima hatua inayosababisha kuazimishana kadi, kutokuwa na kiupaumbele cha bima ya afya kama ajenda ya kudumu.

Baadhi ya wanafunzi waliohudhuria kikao hicho walitoa shukurani kwa mfuko wa NHIF na kuahidi kutumia vyema elimu waliyoipata ili kunufaika na huduma ya matibabu inazotolewa kupitia mfuko huo.

SOMA>>>DC Nyamagana akabidhi Bima za NHIF kwa madereva na Makondakta 

Recommended for you