Michezo

Michuano ya Lake Zone Pre-Season Tournament kutimua vumbi mwezi huu Jijini Mwanza

on

Judith Ferdinand, BMG

Mashindano ya Lake Zone Pre-Season Tournament mwaka 2018 yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 04 hadi 15 katika uwanja mkongwe na wa kisasa wa Nyamagana Jijini Mwanza.

Mwakilishi wa Kamati ya Maandalizi  ya Mashindano hayo, Cuthbert Japhet  anasema yamelenga kuzipa nafasi timu za Kanda ya Ziwa kujiandaa na ligi za kitaifa ikiwemo daraja la kwanza, la pili na ligi kuu kwa msimu huu kwani timu nyingi hazipati nafasi ya kucheza mechi za kirafiki.

Japhet anasema mashindano hayo yameandaliwa na  Cleverland Company Ltd wakishirikiana na Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA) na mpaka sasa timu nne zimethibitisha kushiriki  ikiwemo Mbao FC ambayo ndio wenyeji, Mwadui FC, Kagera Sugar na GPCO huku wakiendelea kufanya mazungumzo na baadhi ya timu kama Biashara FC na Singida United.

Anasema kila timu zitacheza michezo mitatu na mshindi atapatikana kwa atakayekuwa na pointi nyingi  ambapo atapatiwa kikombe na wapili atapata medali huku sehemu mapato yatakayo patikana wakipelekwa kama msaada katika kituo cha watoto wenye ualbino cha Mtindo na cha Wazee Bukumbi.

Naye mwakilishi wa MZFA, Erastus Mayala anawahimiza wadau wa soka kujitokeza kwa wingi kwenye mashindano huku akisema hiyo ni fursa nzuri kwa timu shiriki kujiandaa kuelekea msimu wa ligi kuu Tanzania  Bara pamoja na ligi mbalimbali.

Recommended for you