Michezo

MKUMBA: TUKO TAYARI KWA MECHI YA SIMBA NA YANGA CCM KIRUMBA

on

Na Masyenene Damian

UWANJA wa CCM Kirumba uliopo jijini Mwanza unaomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ulijengwa mwaka 1980 na una uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000, uwanja huo unatajwa kuwa wa pili kwa ukubwa Tanzania Bara baada ya ule wa Taifa, Dar es Salaam wenye uwezo wa kubeba watazamaji 60,000.

Uwanja huo umewahi kukaribisha mechi kubwa za ligi za ndani na mechi za kimataifa, ambapo mechi ya mwisho ya Kimataifa ilikuwa ni ya Julai 15, mwaka huu baina ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na Rwanda kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya kufuzu michuano ya Mataifa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Idadi ya watazamaji

Kwa mujibu wa Meneja wa Uwanja huo, Jonathan Mkumba, uwanja huo una uwezo wa kubeba watazamaji hadi 30,000.

“Uwanja wetu umeanza kutumika kuanzia mwaka 1980 na una uwezo wa kuchukua watu 30,000 kwa utaratibu wetu Waafrika lakini kwa kufuata kanuni kulingana na maelekezo ni watu 25,000,  wakati jukwaa kuu lina uwezo wa kubeba watu 500-600, sijafuatilia rekodi kutoka mwaka 1980 idadi kubwa ya mashabiki kuwahi kuingia lakini kwa kumbukumbu za karibuni mechi ya Alhamisi Mbao dhidi ya Simba ndiyo ilikuwa na mashabiki wengi.

“Rekodi zilizopo ni za miaka ya hivi karibuni, ambapo mwaka jana Simba vs Toto Africans mchezo wa ligi kuu tuliingiza mashabiki 11350, lakini mchezo ulioongoza ni wa wiki iliyopita Septemba 21, mwaka huu kati ya Mbao dhidi ya Simba waliingia mashabiki 12, 300. Mechi za nyuma taarifa zake hatuna kwasababu huwa zinapelekwa makao makuu na mimi nimeingia kazini nina miezi sita nimejaribu kufuatilia naona imekuwa ngumu kupatikana,” alisema Mkumba.

 

Mbao dhidi ya Simba

Katika mchezo huo wa ligi kuu raundi ya nne timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2, mchezo huo unatajwa kuhudhuriwa na watazamaji wengi zaidi ambapo uliingiza kiasi cha Sh milioni 60 kutoka kwa watazamaji 12,300 wakiwemo wa jukwaa kuu 600.

“Zilitengenezwa tiketi 15,000 za jukwaa kuu (VIP) ambazo zilikuwa zinauzwa Sh 20,000 zilikuwa 100, za Bandani zilizokuwa zikiuzwa Sh 10,000 zilitengenezwa 200 kwasababu jukwaa kuu lina uwezo wa kubeba watu 500 na mzunguko za Sh 5,000 zilikuwa 13,000…Kiufupi inakuwa ngumu kukadiria kiasi kamili kwasababu hivi vilabu vikubwa vimekuwa na michezo michafu ya kuchakachua tiketi na umekuwa mchezo wa muda mrefu na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania),” alisema Meneja huyo.

Changamoto

Kwenye mapato timu nyingi zinaleta ujanja tunalazimika  kuingia hasara mashabiki wao wanaharibu miundombinu kama kung’oa koki za maji na uaharibifu mwingine.

Watu na taasisi nyingi hutumia ushawishi wa kifedha kutaka kuingilia mpangilio wa ratiba na matumizi ya uwanja wetu, wanaweza kuleta kiasi kikubwa cha fedha ili achukue siku ambayo amepangiwa mtu mwingine nashukuru hilo nimelithibiti vizuri na nimeliwekea msimamo sana  kwasababu naheshimu ratiba ya kila mtu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Majukwaa

Tofauti na viwanja vikubwa ambavyo majukwaa yana majina, uwanja huu bado majukwaa yake hayajapewa majina lakini huwa yanafahamika tu kwamba kuna jukwaa la mashabiki wa Simba, Yanga ambao huchangia jukwaa na Toto na Mbao FC.

Meneja wa uwanja wa CCM Kirumba, Jonathan Mkumba, aliliambia BINGWA kwamba wanafikiria kuyatambulisha majukwaa hayo kwa kuyapaka rangi zinazofanana na timu husika.

“majukwaa yetu hayana majina lakini tunafikiria kuyaboresha zaidi mbeleni ambapo tunalenga kuyapaka rangi kuendana na rangi za timu husika, kwasasa tunaendelea kuboresha kwa nje tukimaliza huko nje ndiyo tutaingia humu ndani,” alisema Mkumba.

Mechi ya watani wa jadi

Baada ya serikali kuufunga uwanja mkuu wa Taifa, Dar es Salaam ili kupisha ukarabati na matengenezo yanayotarajiwa kukamilika baada ya miezi mitatu, ambapo imezua maswali ni wapi mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga watachezea.

Mechi hiyo inayotajwa kutazamwa na watu wengi zaidi nchini na ukanda wa Afrika Mashariki itapigwa jumamosi ya Oktoba 28, mwaka huu, uongozi wa Uwanja wa CCM kirumba umesema uko tayari kuwakaribisha magwiji hao wa soka katika dimba lake, hasa wakijivunia zaidi baada ya kupitishwa na Shirikisho la Soka duniani (FIFA) na lile la Afrika (CAF) Aprili mwaka huu kutumika mechi za kimataifa.

Meneja wa uwanja huo, Jonathan Mkumba alisema kwamba wako tayari kwa kila kitu na watatumia mwanya wa kufungwa uwanja wa Taifa kuzungumza na bodi ya ligi ili kuileta mechi hiyo jijini Mwanza.

“Tuko tayari mechi iletwe kwenye uwanja wetu kwasababu tunatosha na tumekamilika kwa kila kitu kwasababu uwanja wetu utamudu idadi ya mashabiki na tunafikiria kufanya mazungumzo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili waje Mwanza,” alisema meneja huyo.

Matumizi nje ya soka

Uwanja huo unatumika kwa shughuli mbalimbali nje ya soka ambapo shughuli za kijamii, mikusanyiko na matamasha mbalimbali yamekuwa yakifanyika kwenye uwanja huo na kuleta hofu na kuharibika kwa uwanja hasa eneo la kuchezea (pitch), hata hivyo, meneja Mkumba alisema hawatositisha shughuli nyingine kufanyika uwanjani hapo kwasababu zinawaingizia kipato.

“Ndiyo tumekuwa tukikaribisha shughuli nyingine nje ya soka kwasababu sisi ni wafanyabiashara na lazima uwanja utuingizie pesa na kwakweli soka halituingizii kipato kama ilivyo kwa shughuli zingine kikubwa tunakuwa makini kuhakikisha ‘pitch’ haiharibiki na mara nyingi tunawahimiza wasifanyie katikati ya uwanja,” alisema Mkumba.

Recommended for you