Audio & Video

Wanaume wahimizwa kuwa tayari kupima virusi vya Ukimwi

on

George Binagi-GB Pazzo @BMG

Mkutano wa siku mbili wa wadau wa mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi mkoani Mwanza, umetamatika Jijini Mwanza kwa wadau hao kukubaliana maazimio kadhaa ikiwemo kuwahamashisha wanajamii hususani wanaume kuwa tayari kupima afya zao.

Mkutano huo ulioandaliwa na shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI), uliwashirikisha waratibu wa Ukimwi ngazi za wilaya pamoja na vikundi vya kijamii (CBO) vinavyosaidia mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Afisa Mradi Huduma Unganishi kwa Jamii kutoka shirika la AGPAHI mkoani Mwanza, Cecilia Yona amesema mkutano huo ulilenga kujadili shughuli mbalimbali zinazofanywa na wadau hao na kuweka mikakati ya kuboresha huduma za tiba na matunzo kwa wateja wanaopata huduma katika vituo vya CTC.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wametoa rai kwa wanajamii hususani wanaume kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara na kwamba elimu waliyoipata wataitumia kuwaelimisha wanajamii wengine.

Mkutano huo wa siku mbili kuanzia April 30 hadi jana Mei Mosi, 2018 ulifanyika katika ukumbi wa Adden Palace Hotel Pasiansi Jijini Mwanza, ukihusisha washiriki kutoka wilaya za Nyamagana, Ilemela, Ukerewe pamoja na Sengerema chini ya uratibu wa shirika la AGPAHI linalosaidia mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi nchini kwa ufadhili wa serikali ya Marekani kupitia shirika la Centres for Disease Control (CDC).

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakimsikiliza Afisa Mradi Huduma Unganishi kwa Jamii kutoka shirika la AGPAHI mkoani Mwanza, Cecilia Yona. Bonyeza HAPA ufunguzi wa mkutano huo.

Recommended for you