Audio & Video

Mkuu wa Mkoa Mwanza atekeleza agizo la Rais Magufuli

on

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe.John Mongella ametekeleza agizo la Rais Mhe. Dkt. John Magufuli la kuhakikisha anafuatilia kero za wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga) na kuzitafutia ufumbuzi.

Katika kutekeleza agizo hilo, Mhe. Mongella amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Sengerema Magesa Mafuru kuhakikisha anakutana na wafanyabiashara wadogo (machinga) ambao walinyang’anywa matunda yao (nanasi) zao kwenye oparesheni ya kuwaondoa barabarani ili walipwe fidia.

Hatua hiyo ilijiri jana Agosti 18, 2018 baada ya Mhe. Rais Dkt. Magufuli akiwa njiani Mjini Sengerema akielekea Chato mkoani Geita kwa ajili ya mapumziko, kutoa agizo kwa watendaji wa halmashauri hiyo kutowasumbua machinga na badala yake wawache wafanye biashara zao huku akiagiza watendaji nchini kujikita kutatua kero za wananchi.

Ni baada ya Mhe. Rais Dkt. Magufuli kusimama kwa ajili ya kusalimiana na wananchi ambapo wafanyabiashara ndogo ndogo walimueleza kero zao ikiwemo ukosefu wa maeneo ya kufanyia biashara zao hatua inayosababisha kubugudhiwa na viongozi wa halmashauri.

Kufuatia malalamiko hayo, Mhe. Rais Dkt. Magufuli alimuagiza Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. John Mongella kufuatilia kero hizo na kuzitatua ambapo muda mfupi baadaye Mhe. Mongella alikutana na viongozi mbalimbali wilayani Sengerema akiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi pamoja na machinga kwa ajili ya kutekeleza agizo la Mhe. Rais Dkt. Magufuli.

Meza za wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) katika soko la Kisima cha Chumvi Mjini Sengerema ambalo limetengwa kwa ajili ya wafanyabishara hao. Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara wanagoma kuhamia katika soko hili kwa kile wanachodai ni kukosa wateja na hivyo kuendelea kufanyia biashara zao katika hifadhi ya barabara Mjini Sengerema.

Tazama BMG Online Tv hapa chini

PIA SOMA Hii ndiyo miradi kabambe ya maendeleo wilayani Sengerema

Recommended for you