Michezo

Morning Star yafuzu nusu fainali michuano ya Ndondo Cup Jijini Mwanza

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ndondo Cup 2017, imekamilika kwa timu ya Morning Star kufanikiwa kufuzu kuingia nusu fainali baada ya kuichapa Phantom Fc goli 7-6 katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Mchezo huo  ambao umekua ni wa mwisho katika hatua hiyo, mpaka dakika 90 zinamalizika hakuna  timu iliyoweza kuona lango la mwenzie na kupelekea kucheza kwa penati(matuta), ambapo tangu kuanza kwa hatua ya robo fainali ya mashindano hayo, hiyo ndio imekua mechi ya kwanza kucheza matuta.

Timu zote zilifanikiwa kupiga penati 7, huku Morning Star wakifunga zote na Phantom Fc wakifanikiwa kufunga 6 na kupoteza moja, na kupelekea kushindwa kufuzu kuingia nusu fainali.

Wachezaji wa Morning Star waliopiga penati ni Joshua Bundala,Baraka Mange,Masunga Thomas, Demanus Kalegea,Jofrey Joshua,Khamis Kasa,Silias Mashine huku Phantom Fc   ni  Robert Magadula,Frank Dimati,Carlos Protus,Ally Msengi,Frank Sekule,Dotto Bryton pamoja na Abdalah Mohammed aliyekosa penati.

Hata hivyo Joshua Bundala ambaye ni Nahodha wa timu ya Morning Star ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo, na kujinyakulia kitita cha shilingi 30000 kutoka HASFU Barber Shop.

Bundala alisema, anamshukuru Mungu kwa ushindi walioupata,hivyo wamejipanga kufanya vizuri hatua ya nusu fainali na fainali, pia wanapambana  kuonyesha vipaji vyao ili waweze kufikia  malengo yao.

Kwa upande wake Kocha wa Morning Star Wilbert Mwita alisema, wamejianda siku zote na vijana wamecheza vizuri na kufanikiwa kuibuka na ushindi, hivyo wanajipanga kufanya vizuri zaidi hatua zinazofuatia na kuibuka mabingwa, na mashabiki wasikate tamaa ili kuendeleza soka mkoa wa Mwanza.

Naye Kocha wa Phantom Fc Godfrey Chapa alisema, wamepoteza mchezo kwa kukosa penati moja hali iliyopelekea kushindwa kufuzu kuingia nusu fainali na kuwapongeza vijana wake kucheza vizuri dakika 90 za mchezo.

Hata hivyo, akizungumzia changamoto ya mashindano hayo, alisema, waamuzi wanatakiwa kuchezesha mechi kihalali na kufuata Sheria, maana katika mchezo huo  mwamuzi akuwatendea haki kwa kumpa kadi nyekundu mchezaji wa timu yao Darlington Enyina dakika ya 33 baada ya kuwatukana mashabiki, ikiwa ni kosa la kwanza na halipaswa kuonywa na siyo kutolewa nje ya uwanja.

Recommended for you