Habari Picha

Walengwa mkoani Geita wanufaika na mabilioni ya TASAF

on

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameendesha kikao cha tatu cha Tathimini ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini nchini TASAF awamu ya tatu ambacho hufanyika mara moja kila mwaka tangu kuanza kwa mpango huo.

Akizungumza jana kwenye kikao hicho, Mhandisi Gabriel alianza kwa kuwapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kutoa taarifa sahihi lakini pia kuwashukuru waratibu wa mpango huo kuanzia ngazi ya Sekretarieti ya Mkoa hadi ngazi za Halmashauri na kusema kuwa, ni imani yake kikao hicho kitaweka mikakati thabiti ili kupata matokeo chanya. Ni baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa mpango huo,ndani ya ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Mkuu wa Mkoa aliendelea kwa kusema “nimeona mabadiliko makubwa ,nimefurahishwa na mashamba ya pamba ambayo yanamilikiwa na walengwa wa mpango. Nawashukuru sana viongozi kwa usimamizi mzuri, hivyo ni vyema viongozi kuendelea kuzitembelea kaya hizi na kila mmoja kwa nafasi yake, kwenye eneo lake, ahakikishe TASAF awamu hii inakuwa yenye manufaa kwenye eneo husika lakini walengwa wanaondokana na umasikini kupitia ufuatiliaji wa karibu ili nia ya Serikali ya Awamu ya Tano iendelee kufanikiwa”.

Akisoma taarifa ya utekelezaji, Mratibu wa TASAF ngazi ya Mkoa Bw. Elikana J. Harun alieleza kuwa, Mkoa wa Geita umehawilisha jumla ya Shilingi Bilioni Ishirini na Tatu, Mia Sita Themanini Milioni, Sitini na Nane Elfu na Hamsini na Nane  (Tshs.23,680,068,058) sawa na asilimia 98.32 ya fedha zilizopokelewa ili kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini – TASAF awamu ya Tatu kuanzia Julai 2015/2016 hadi Juni, 2017/2018, kazi iliyofanyika kwa vipindi 18 katika Mitaa 27 na Vijiji 321 vilivyoingizwa kwenye mpango huo kwenye halmashauri sita za Mkoa wa Geita.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TASAF Bw. Zacharia Ngoma alipongeza kasi ya Geita baada ya michango iliyotoka kwa waheshmiwa wakuu wa Wilaya za Geita ambao pia walihudhulia akiamini kama viongozi wana uelewa mzuri wa mpango huo, basi utafanikiwa; kisha kuwakumbusha kuzitembelea kaya maskini vijijini ili kujifunza mengi zaidi.

Mkuu wa Mkoa Geita (kushoto) pamoja na Mkuu wa Wilaya Geita (kulia) wakiwa kwenye kikao cha TASAF

Katibu Tawala Mkoa Geita, Selestine Gesimba akizungumza kwenye mkutano huo

Zacharia Ngoma ambaye ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TASAF akizungumza kwenye mkutano huo

Viongozi mbalimbali pamoja na washiriki wa mkutano huo. Imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita

Recommended for you