Habari Picha

Shirika la KCBRP lazindua mradi jumuishi kwa watu wenye ualibino Misungwi

on

Judith Ferdinand, BMG Habari

Katika kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za serikali za  kutatua  changamoto mbalimbali  za watu wenye ualibino na kuwalinda shirika la Karagwe Community Base Rehabilitation Programmes (KCBRP) wamezindua Mradi Jumuishi wa watu wenye Ualbino wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Uzinduzi  wa mradi huo ulienda sanjari na semina ya uhamasishaji kulinda na kutetea haki za watu wenye ualbino iliyofanyika juzi katika ukumbi  wa  kanisa la Romani Katoliki wilayani Misungwi.

Meneja Mradi wa mradi huo, Florence Rugemarika kutoka shirika la KCBRP linalojishughulisha na watu wenye ulemavu, alisema mradi huo umejikita katika mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Geita,Shinyanga,Kagera na Simiyu wenye gharama ya bilioni 2.4, ambao umeanza 2017 hadi 2020 wakishirikiana na shirika la Under the Same Sun na  Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS).

Rugemarila alisema lengo la mradi huo ni kuondoa mila na desturi potofu kwa jamii zinazosababisha kuwatendea vitendo vya ukatili watu wenye Ualbino na kutambua walipo na idadi yao ili kuweza kuwatimizia mahitaji yao pamoja na kuwalinda.

Alisema kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya watu hao, kujenga uwezo kwa taasisi zinazojishughilisha na watu wenye Ualbino ili zijisimamie na kujiendesha zenyewe pamoja na kutoa huduma moja kwa moja  zinazokidhi mahitaji yao ikiwemo mafuta ya kuzuia mionzi ya jua.

Pia alisema anashukuru serikali kwa kutoa mafuta ya kuzuia mionzi ya jua kwa watu wenye Ualbino na amehakikisha kuwa kwa Kanda ya Ziwa wale wote wanaowafikia kuyapa,hivyo kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine wameweza kuwajengea nyumba wale waliokuwa na uhitaji na wataendelea kufanya hivyo.

Hata hivyo alisema KCBRP haiwezi pekee yake kuwawezesha kiuchimi bali wanashirikiana na taasisi zingine kwa kuwapa mafunzo ya muda mfupi ya ujasiriamali kisha kuwaunganisha na halmashauri ili kupatiwa mikopo na kuweza kufanya shughuli za uzalishaji pia wataendelea kuhamasisha wadau wa ndani na nje ya nchi ili kusaidia kipata mafunzo ya muda mrefu katika masomo yao na baadae kupata madaktari na wataalamu katika nyaja mbalimbali kutoka kundi hilo.

Naye Mwenyekiti wa  TAS wilaya ya Misungwi Chalya Saguja alisema, kutoka na jamii kuwa na mtazamo hasi juu yao imepelekea na wao kutojitambua na kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi hali inayopelekea kuwa na maisha duni na kushindwa kufikia huduma za muhimu hasa za kiafya.

Pia alimuomba Mkuu wa wilaya hiyo kuwajengea mazingira mazuri wale ambao wapo kwenye makao maalumu waweze kujitegemea pamoja na wizara ya elimu  isaidie watoto wenye Ualbino waende shule kwani elimu ndio itakayowasaidia kuondokana na changamoto na utegemezi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda alisema, serikali ipo makini kuhakikisha usalama na hakutakuwa na mtu atakayepoteza  maisha kwa imani za kishirikina wakiwemo kundi hilo, kwa upande wa  ulinzi wapo vizuri kuanzi ngazi ya vitongoji hadi wilaya na Mungu atawasaidia.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi, Eliurd Mwaitekeleka alisema walemavu katika halmashauri hiyo likiwemo kundi hilo waunde vikundi ambavyo vipotayari kuleta mabadiliko kiuchumi na watapatiwa mkopo wa asilimia tano kama makundi mengine pamoja na kumuhamishia Mwenyekiti TAS Misungwi mjini ili kurahisisha utendaji na utekelezaji majukumu kwa watu wenye Ualbino.

Hata hivyo Katibu wa Madiwani halmashauri ya Misungwi Charles Kaphipa alisema suala la kulinda na kutetea watu wenye Ualbino ni jukumu la wote hivyo lazima kuhakikisha tunatekeleza wajibu.

Aidha Afisa Ustawi wilaya ya Misungwi, Godfrey Vedasto alisema wataendelea kutoa elimu katika jamii ili kuondoa unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu, kuandaa maandiko ili kuwashawishi wadau mbalimbali kushiriki kuwakwamua kiuchumi pamoja na kushirikiana na KCBRP kupitia mradi huo kuwatambua watu wenye Ualbino na kufahamu mahitaji yao halisi.

Vilevile mmoja wa  watu wenye Ualbino Zabibu Abdalah alisema ujio wa mradi huo utawafanya waweze kutambulika na kuthaminiwa kwenye jamii,kupata elimu pamoja na mahitaji yao muhimu hasa ya kiafya.

Recommended for you