Audio & Video

Waziri wa Afya azindua mradi wa TUWATUMIE Itilima mkoani Simiyu

on

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amezindua rasmi mradi wa TUWATUMIE unaotekelezwa katika wilaya za Itilima mkoani Simiyu na Misungwi mkoani Mwanza.

Uzinduzi wa mradi huo unaotekelezwa na shirika la Amref Health Africa Tanzania pamoja na taasisi ya Benjamin Mkapa umefanyika hii leo katika wilaya ya Itilima, ukilenga kuboresha huduma za afya hususani huduma za uzazi ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto chini ya miaka mitano.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri Mwalimu amesema serikali itaendelea kuboresha huduma za afya ikiwemo kuongeza watumishi wa afya pamoja na kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili wasaidia kutoa huduma za afya kwa wananchi.

Naye Mkuu wa Miradi kutoka shirika la Amref Health Africa Tanzania, Dkt.Aisa Muya amesema utekelezaji wa mradi wa TUWATUMIE unaofadhiliwa na serikali ya Ireland kupitia shirika la Irish Aid, ulianza mwezi Disemba 2017 na unatarajiwa kufikia tamati mwezi Juni mwaka 2020 ambapo ametoa rai kwa serikali kuandaa mwongozo utakaowaajiri wasaidizi hao wa afya ngazi ya jamii baada ya kipindi cha mwaka mmoja ambacho shirika hilo litakuwa likiwalipa mishahara kukamilika.

Amesema mradi huo ulibuniwa na shirika la Amref Health Africa Tanzania kwa kushirikiana na taasisi ya Benjamin Mkapa pamoja na Wizara ya Afya kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma (Health Promotion Unit) lengo likiwa ni kuajiri watumishi wapatao 215 wilaya za Itilima na Misungwi (Itilima wahudumu 102 na Misungwi wahudumu 113) ili wasaidie utoaji huduma za awali kwa wananchi.

“Asilimia 50 ya miradi yetu inatumia watoa huduma za afya ngazi ya jamii ambapo kwa mwaka huu tayari wahudumu 2,265 wamepatiwa mafunzo na majukumu yao makubwa yanaanza kwa kuwahamasisha wananchi kuzingatia usafi wa mazingira, utumiaji wa maji safi na salama, kuzuia ukatili wa kijinsia, kutoa elimu ya lishe bora, kutambua viashiria vya magonjwa hatarishi kwa akina mama”. Amesema Dr.Muya.

Nao baadhi ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii wilayani Itilima wamesema wako tayari kufanya kazi kwa bidii na weledi hususani kuwahamasisha wananchi kuhudhuria kliniki, kujifungulia katika vituo vya afya ili lengo la kupunguza vifo vya akina mama na watoto chini ya miaka mitano liweze kutimia.

Waziri Ummy Mwalimu akibonyesha alamu kuashiria uzinduzi wa mradi wa TUWATUMIE unaolenga kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kusaidia upatikanaji wa huduma za afya ili kupunguza vifo vya mama na mtoto

Waziri Mwalimu akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi wa TUWATUMIE

Wawakilishi mashirika mbalimbali akiwemo Mkuu wa Miradi kutoka shirika la Amref Health Africa Tanzania, Dkt.Aisa Muya (katikati) wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi huo

Baadhi ya wanachi wakifuatilia uzinduzi huo

PIA SOMA Wanahabari Simiyu kushirikiana na Amref kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi

Recommended for you