Audio & Video

Wananchi waomba mradi wa maji Buyagu Sengerema ukamilike kwa wakati

on

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Wakazi wa Kijiji cha Buyagu katika Halmashauri ya wilaya Sengerema mkoani Mwanza wameiomba serikali kusimamia vyema mradi wa maji wa Buyagu-Kalangalala-Bitoto ili ukamilike kwa wakati na kuwawezesha kupata maji safi na salama.

Wakazi hao waliyasema hayo jana baada ya Kamati ya Siasa (CCM) Mkoa Mwanza ikiongozwa na Mwenyekiti wake Dkt.Antony Diallo ili kujionea utekelezaji wa mradi huo ambao ulianza tangu Januari 2014 ukitekelezwa na kampuni ya “D4N Co. Ltd” kwa gharama ya shilingi bilioni 1,702,500,170.

Mkandarasi wa mradi huo ambao chanzo chake ni maji ya Ziwa Victoria alieleza kwamba umechelewa kukamilika kutokana na ucheleweshwaji wa fedha ambapo hadi sasa fedha zilizotolewa na serikali ni shilingi milioni 661,648,480 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 70 ambapo ukikamilika utawahudumia zaidi ya wakazi 16,000 waishio Vijiji vya Buyagu, Kalangalala na Bitoto.

Awali Kamati hiyo ilitembelea Kituo cha Afya Kome kilichopo Halmashauri ya Buchosa kinachotekeleza mradi wa ujenzi wa majengo ya upasuaji, maabara, wodi ya wazazi, chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na nyumba mbili za watumishi kwa gharama za shilingi milioni 400 zilizotolewa kupitia mpango wa malipo kwa ufanisi (RBF) na kuridhishwa na utekelezaji wake.

Miradi mingine iliyokaguliwa na Kamati hiyo ni mradi wa maji Lumeya-Kalebezo-Nyehunge uliopo Halmashauri ya Buchosa pamoja na chanzo cha maji Busisi Halmashauri ya Sengerema ambapo Mwenyekiti Dkt.Antony Diallo alitoa maelekezo kwa wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili kutoa huduma kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa (CCM) Mkoa Mwanza Dkt.Antony Diallo (katikati) akizungumza na Mhandisi wa Maji Sengerema (kushoto) baada ya Wajumbe wa Kamati hiyo kutembelea mradi wa maji wa Buyagu-Kalangalala-Bitoto. Kulia ni Mkuu wa Mkoa Mwanza ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe.John Mongella

SOMA Kamati ya Siasa Mkoa Mwanza yakagua miradi ya maendeleo Halmashauri ya Buchosa

Recommended for you