Audio & Video

Baraza la Watoto mkoani Mwanza latoa rai kwa wazazi

on

Judith Ferdinand, BMG

Wananchi wamehimizwa kuendelea kuchangia uboreshaji wa miundombinu ya elimu ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya maabara ili kuwawezesha wanafunzo kusoma kwa nadharia na vitendo.

Mwenyekiti wa Baraza la Watoto mkoani Mwanza, Neema Theonest alitoa rai hiyo jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, yaliyofanyika katika viunga vya shule ya Sekondari Sangabuye Manispaa ya Ilemela.

Alisema serikali inajizatiti kuboresha miundombinu ya elimu hivyo wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano wao ikiwemo kuchangia ununuzi wa vifaa vya maabara ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora na hatimaye kufikia uchumi wa viwanda kama kauli mbiu ya maadhimisho hayo inavyosema “Kuelekea uchumi wa viwanda, tusimuache mtoto nyuma”.

Naye Mganga Mkuu Mkoa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa alisema jamii inapaswa kuelimishwa ili kutoa ushirikiano kwenye uboreshaji wa miundombinu ya elimu huku akitoa rai kwa kila mmoja kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pale panapotokea masuala ya unyanyasaji kwa watoto.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Plan International mkoani Mwanza, Baraka Mgohamwende ili kufikia uchumi wa viwanda na kuwa na jamii salama watoto wanapaswa kuacha kuiga tamaduni za kigeni huku serikali ikiimarisha ushiriki kwa watoto katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu bora.

Meneja Mradi wa Shirika la Railway Children Africa, Abdalah Issa alisema sababu ya kuadhimisha siku hiyo ni kuikumbusha jamii kuacha kufanya vitendo vya unyanyasaji na pia kuwakumbuka watoto takribani 600 waliouwawa Afrika Kusini wakiandamana kudai haki zao.

Alisema ili kuonyesha umuhimu wa mtoto na haki zake ikiwemo kulindwa, kupatiwa malezi bora, elimu, kushirikishwa katika masuala mbalimbali kama sera ya mtoto inavyoelekeza na kuongeza kwamba mwaka 2015/16 watoto waliokuwa wakiishi mtaani ni 1940, mwaka 2017 ni 1924  na vijana 499 miongoni mwao wanafanya biashara za kutumikishwa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Mwanza.

Mwanasheria wa shirika la Wadada Center For Solution Focused Approach, Anitha Samson alisema wazazi na walezi wanapaswa kuungana pamoja katika suala la malezi bora na kujiepusha na migogoro ambayo husababisha watoto kukosa malezi pindi familia zinapotengana.

SOMA PIA Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mkoani Mwanza

Recommended for you