Audio & Video

“Mwaka mmoja bila Mama, nimejifunza Kupenda”-George Binagi

on

Mwaka mmoja bila uwepo wa mama mzazi na rafiki yangu kipenzi, nimejifunza KUPENDA ZAIDI. Nasema hivyo kwa maana ya kumpenda yeyote na kumtendea mema wakati wote lakini kubwa zaidi kuwapenda akina mama.

Ni kweli leo hii mama yangu kipenzi ametangulia mbele za haki, lakini nimejifunza kumpenda mama yeyote yule maishani mwangu. Inawezekana hutambui umuhimu wa mama ndiyo maana umemtelekeza ama unamdharau, jibu ni dogo sana, unafanya hivyo kwa sababu hujui umuhimu wake. Subiri Mungu amchukue ndo utatambua niyasemayo.

Daima naikumbuka sana kauli ya mama yangu Leah Binagi “Mwanangu inabidi sasa uoe bado nikiwa na nguvu”. Kauli hii aliniambia mwaka 2014. Nilimwahidi kufanya hivyo.

Mwaka 2015 na 2016 kukawa na mwingiliano wa ratiba nyingine mbili za harusi za wadogo zangu na wakati huo mama akawa ameanza kuandamwa na maradhi. Siku moja akiwa amelala kitandani hawezi hata kuamka, nikamwambia “mama siku nikija umeamka na kutembea mwenyewe, nitakwambia tarehe ya mimi kuoa maana natamani ushuhudie harusi yangu”.

Kuna siku nikaenda kumsalimia na nikamkuta na tabasabu kubwa na akaniambia “hivi sasa nasimama na hata leo nimeoga mwenyewe, hivyo niambie unaoa lini?”. Kwa kweli siku hiyo nilifurahi na tukaanza kupanga mipango ya harusi na mwezi wa 10 mwaka 2016 nikaenda ukweni kujitambusha.

Baadaye mipango ya harusi ikaanza na tukakubaliana kufanya harusi tarehe 26.02.2017 lakini baadaye nikasogeza mwezi mmoja mbele ili afya ya mama iimarike zaidi na aweze kufurahia harusi yangu na harusi ikapangwa 26.03.2017.

Jumapili Januari 29,2017 baada ya ibada, tukaanza kikao cha kwanza cha harusi yangu Jijini Mwanza. Bila kujua kwamba hali ya mama imeanza kubadilika akiwa nyumbani Tarime. Tulimaliza kikao vizuri na ilipofika saa 12 jioni nikiwa na rafiki zangu tukifurahia, simu yangu ikaita na sikuipokea, ikaita tena sikuipokea, mara ya tatu rafiki zangu wakaniambia wee ipokee tu.

Ilikuwa simu ya binamu yangu akiniambia hali ya mama si nzuri hivyo kesho niwahi nyumbani. Nilitamani sana kuanza safari lakini kwa muda ule nisingeweza kupata usafiri wa kutoka Mwanza kwenda Tarime hivyo nikapanga kuanza safari kesho yake, na mwili wangu ukakosa kabisa amani hivyo nikarejea nyumbani (Mwanza) na rafiki zangu.

Sikuamini usiku majira ya saa tano nilipopokea simu kwamba kipenzi changu, mama yangu amefariki. Siwezi kuelezea zaidi maumivu niliyoyapata lakini inatosha tu kusema “niliumia, ninaumia na nitaendelea kuumia” kwani mama aliondoka katika muda ambao bado mimi na ndugu zangu tulikuwa tukimtegemea sana, si kwa jambo lolote lile bali uwepo wake tu.

Niliumia kwani mama alifariki siku ambao nilianza kikao changu cha kwanza cha harusi yangu, labda nafsi yake iliridhika na ikaona hakuna umuhimu wa kusubiri sherehe. Namshukuru Mungu tulimhifadhi salama mama na ndoa ilifanyika ingawa kwa ugumu sana. Nawashukuru nyote kwa upendo wenu.

“Mwaka mmoja bila mama, hakika nimejifunza kupenda zaidi, kuwapenda akina mama, kumpenda mama wa mwenzangu kwani najua maumivu ayapatayo mtoto asiye na mama hivyo siwezi kumtendea ubaya. Ninamshukuru Mungu kwa kila hatua, pumzika kwa Amani Mama, Amina!”. George Binagi-GB Pazzo @BMG

Kipenzi changu, nafurahi kwamba mama alitupatia baraka zote kabla ya mauti.

Recommended for you