Michezo

MWANZA: Ibungilo waibuka mabingwa Angeline Jimbo Cup 2018

on

Judith Ferdinand, BMG

Timu ya Kata ya Ibungilo imeibuka mabingwa wa mashindano ya Angeline Jimbo Cup msimu wa 2018/19 baada ya kuilaza Kirumba kwa goli 4-1.

Katika mchezo wa fainali uliotimua vumbi leo kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Ibungilo ilifunga goli dakika ya nane kupitia mshambuliaji wake Yusuph Amran huku Kirumba  ikisawazisha dakika ya 77 na hivyo hadi dakika 90 matokeo yalikuwa 1-1.

Baada ya dakika 90 za mchezo huo, ilifuata mikwaju ya penalt ambapo Ibungilo ilipata mikwaju mine huku Kirumba ikifunga mkwaju mmoja na kukosa mikwaju miwili na hivyo kuibuka mabingwa wa msimu huu.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha wa Ibungilo Swala Daud alisema anamshukuru Mungu kuibuka na ushindi huo pamoja na mashabiki waliojitokeza kuwaunga mkono pamoja na mbunge wa Jimbo la Ilemela  Dkt.Angeline Mabula kwa kuandaa mashindano hayo ambayo yamesaidia vijana kuonyesha vipaji na kuibua vipya ambapo msimu wa 2016 ilishika nafasi ya pili na wanajipanga na msimu ujao.

Naye Kocha wa timu ya Kirumba, Iddi Kilewa alisema wamepoteza mchezo huo baada ya kushindwa kutumia nafasi walizozipata hivyo wanajipanga na msimu ujao huku akimuomba Dkt.Mabula msimu ujao waachie Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza(MZFA) ndio wachezeshe na kusimamia ili kuleta usawa na sheria 17 za mpira zifuatwe.

Kwa upande Dkt.Mabula alisema mashindano hayo yamelenga kuendeleza na kuibua vipaji vipya vinavyopatikana kwenye jimbo lake huku akisisitiza kuwa yatafanyika kila mwaka mara baada ya kupatikana shiriki sanjari na  kuwaomba viongozi na wananchi wa jimbo hilo kuunga mkono jitihada anazozichukua katika kuhakikisha wilaya ya Ilemela inaendelea kuwa kitovu cha  kuzalisha vipaji vya michezo mbalimbali nchini.

Naibu  Waziri Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Athony Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi katika fainali hiyo alimpongeza Dkt.Mabula kwa kuaandaa mashindano hayo kwa ajili ya kuendeleza michezo kwa vijana kama ilivyo dhima ya serikali hivyi aliwaomba wabunge na viongozi wengine kuiga mfano.

Timu ya Ibungilo imejinyakulia kitita cha Milioni mbili, kombe, mpira mmoja pamoja na seti moja ya jezi, mshindi wa pili  timu ya Kirumba imepata Milioni 1.5, kombe,  jezi seti moja na mpira mmoja huku mshindi wa tatu timu ya Shibula ikiibuka na Milioni 1, kombe, mpira pamoja na jezi seti moja.

Recommended for you