Habari Picha

Kichocho na Minyoo bado changamoto mkoani Mwanza

on

Judith Ferdinand, BMG

Zaidi ya watu milioni 1.5 mkoani Mwanza wanatarajiwa kupata dawa za kinga na tiba ya magonjwa ya kichocho na minyoo ambayo yamekuwa hayapewi kipaumbele, kuanzia Agosti 6 hadi 12 mwaka huu.

Akizungumza jana wakati wa kikao cha utekelezaji mipango ya zoezi la ugawaji dawa hizo, Mratibu  wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Mkoa wa Mwanza, Dkt.Mabai Leonard alisema kati ya watu milioni 1.5 wanaotarajiwa kupata dawa hizo, wanafunzi  ni 878,624 kutoka shule za msingi 663 huku 627,917 wakiwa ni wanajamii kutoka Kata 41 za halmashauri tano za mkoa zikiwemo Magu,Ukerewe, Buchosa, Sengerema na Jiji la Mwanza.

“Kuna madhara yanayotokana na magonjwa hayo endapo yasipo patiwa kinga na tiba mapema ikiwemo utumbo kujisokota, saratani ya kibofu cha mkojo, ini pamoja na upungufu  wa damu na utapia mlo hivyo ni fursa kwa wananchi kujitokeza  katika kampeni zoezi hili”. Alisema Dkt.Mabai na kuongeza;

“Katika tathimini ya awali iliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa  ya Binadamu  Tanzania (NIMR), mkoa wa Mwanza una asilimia 81 ya watu wana maambukizi ya kichocho na minyoo hivyo Serikali imekuja na kampeni ya kutoa chanjo ya magonjwa hayo ili kuyadhibiti”. Alibainisha.

Naye Afisa Mpango wa Magonjwa  yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Oscar Kaitaba alisema zoezi hilo litafanyika kuanzia ngazi ya shule ambapo itawahusu watoto wenye umri  kuanzia miaka mitano hadi 14 kwa siku moja ya Agosti 6 na wanafunzi watapatiwa ya Praziquantel kwa ajili ya kichocho na Albendazole  ya minyoo kwa ajili ya kukinga na kutibu.

Alisema kwa upande wa jamii watagawa dawa aina moja ya Praziquantel  kwa ajili ya kichocho kwa watu wenye umri wa miaka mitano na kuendelea pamoja na kuwashauri  kwenda hospitali kupima ili wapatiwe dawa za minyoo na kuzingatia usafi ili kujiepusha na magonjwa hayo.

Naye Mganga Mkuu wilayani Ilemela, Dkt.Florian Tinuga alisema kwenye kampeni hiyo wanatarajia kuwapatia dawa wanafunzi 96,200 waliopo shule  za msingi huku ngazi ya jamii  hawata husika kutokana na mwezi Februari mwaka huu NIMR walitoa  dawa katika maeneo ya ukanda wa  Ziwa Victoria katika wilaya hiyo.

 

Recommended for you