Habari Picha

Naibu Waziri Ulega aagiza uundaji wa Ushirika wa wavuvi Kanda ya Ziwa

on

Judith Ferdinand, BMG

Naibu Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdallah Ulega amewaangiza Maofisa Uvuvi Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanaanzisha ushirika wa wavuvi wadogo wadogo katika mialo mbalimbali  ikiwemo Kigangama wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Ulega alitoa agizo hilo jana alipotembelea Mwalo wa Kigangama uliopo Magu na Chuo cha Uvuvi ( FETA) kituo cha Gabimori wilayani Rorya wakati wa ziara yake katika mikoa ya Mwanza  na Mara.

“Nikirudi hapa baada ya mwezi mmoja nataka nikute ushirika wa wavuvi wadogo wadogo umeanzishwa katika mialo yote ikiwemo ya Kigangama Magu na Sota Rorya, hivyo watendaji katika sekta ya uvuvi pamoja na wakuu wa wilaya mshirikiane kuhakikishe mnasimamia suala hili kwani litawasaidia kuwa na sauti ya pamoja katika msimamo wa bei pamoja na kutatua changamoto zao kama kukopeshwa  mashine na nyavu za kisasa katika kuendeleza kipato binafsi na taifa”. Alisema Ulega.

Alisema oparesheni ya kudhibiti uvuvi haramu inaendelea hivyo wavuvi wafuate sheria, taratibu na kanuni kwani kupitia kampeni hiyo wamegundua mambo mengi ikiwemo namna ambavyo wavuvi wadogo wanavyo nyonywa na wachakataji wa samaki hususani katika bei ambayo huacha maskini huku wenye viwanda wakinufaika zaidi.

“Mvuvi anauza samaki kwa kilo moja shilingi 5,000 ambayo inamuacha masikini wakati anatumia muda na gharama kubwa ya mfuta wakati wa kuvua na kumnufaisha mchakataji ambaye anauza kichwa, ngozi, mnofu, mafuta, mifupa kwa bei kubwa hususani bondo ambalo linauzwa kuanzia 100,000 hadi 600,000 kwa kilo hivyo Serikali inaangalia namna ya kulikomboa kundi hilo ili liweze kunufaika”. Alisema.

Pia Ulega alipata fursa ya kuteketeza zana haramu za kuvulia samaki ikiwemo nyavu, ndoano, kokoro za samaki, dagaa pamoja na kamba.

Naye Afisa Uvuvi Kanda ya Simiyu na Magu, Samson Mboje alisema kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia Agosti hadi Septemba mwaka huu wameweza kukamata  zana za uvuvi haramu ikiwemo makokoro ya samaki 112, ya dagaa 12, nyavu za samaki 78, kamba za kokoro 52,500 ambavyo Naibu Waziri ameviteketeza na kwamba ndoano 5,500 zinaombewa kibali mahakamani ili kuziyeyusha katika kiwanda cha Nyakato Steel kwani ni chuma.

Naye Katibu wa BMU mwalo wa Kigangama, John Masato alisema wanakabiliwa na wizi wa zana za uvuvi ziwani pamoja na kuuzwa kwa bei ghali na kushuka kwa bei ya mazao ya samaki.

Aidha Mwenyeikti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Albert Machiwa aliiomba Serikali kuongeza ulinzi kwa kufanya doria ziwani hususani katika maeneo yaliyopakana na nchi jirani za Kenya na Uganda ambapo askari wao pamoja na watanzia wachache wasio waadilifu wamekuwa wakiwapiga wavuvi.

Recommended for you