Habari Picha

Biteko awataka wawekezaji kuandaa mipango ya kuhudumia wanajamii

on

Mwandishi Maalum

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka wawekezaji katika sekta ya madini kuandaa mipango kazi ya namna ya kutoa huduma za maendeleo katika jamii na kuiwasilisha kwa wakurugenzi wa halmashauri husika ili kushirikiana katika kutekeleza mipango hiyo.

Biteko alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uchimbaji madini katika Kijiji cha Maseyu mkoani Morogoro.

Aidha Biteko alikemea tabia za baadhi ya viongozi wa serikali kuomba kwa wawekezaji kwa ajili ya kuendeshea vikao na badala yake wawe na mipango ya kimaendeleo.

Alisema wawekezaji katika eneo husika wanapaswa kusaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati, shule na barabara miradi ambayo itakuwa ikikumbukwa hata baada ya madini kuisha katika maeneo hayo.

Aliwaasa wananchi na viongozi kutumia kodi zinazotokana na uwekezaji huo katika kutekeleza miradi yenye tija na kueleza kuwa madini yana mwisho hivyo ni vyema kuhakikisha kuna miradi endelevu itakayosalia kama kumbukumbu.

Recommended for you