Habari Picha

Ndoa za utotoni bado changamoto nchini Tanzania

on

Na Mwandishi Maalum

Imeelezwa kwamba watoto wa kike 36 kati ya 100 hapa nchini huolewa chini ya umri wa miaka 18 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali duni ya maisha pamoja na tamaa kwa baadhi ya wazazi hali inayosababisha kuongezeka kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto.

Hayo yalibainishwa Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni  (TECMN) Valerie Msoka, wakati akizungumza kwenye mkutano uliowashirikisha wajumbe wa baraza la mahusiano ya dini mbalimbali kwa lengo la kutokomeza ukatili huo ili kufikia asilimia sifuri.

Alisema licha ya juhudi mbalimbali ambazo wamekua wakizichukua ili kutokomeza changamoto hiyo, bado kuna haja ya kufanyia marekebisho sheria ya ndoa ya 1971 kifungu cha (13) na (17)  kinchoruhusu ndoa chini ya umri wa miaka 18 ambapo imeonekana kuwa ni tatizo kubwa katika kuongezeka kwa vitendo vya ukatili.

Kwa upande wake Mratib wa mtandao huo, Michael Jackson alisema wamekua wakifanya tafiti mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na kuandaa matamasha mbalimbali ambayo yamekua yakilenga kutoa elimu juu ya athari za ndoa za utotoni.

Aidha alisema utafiti uliofanywa na mtandao huo unaonyesha kwamba mikoa inayoongoza kitaifa kwa matukio hayo ni Tabora ambapo kati ya watoto 100 watoto 58 wameolewa chini ya umri wa miaka 18, Shinyanga 59, Mara 55 pamoja na Dodoma 51 hali ambayo hupelekea kuathirika kwa watoto kisaikolojia na kimwili.

Recommended for you