Habari Picha

Ngariba wilayani Tarime wapewa mafunzo ya ujasiriamali

on

Na Frankius Cleophace, Tarime

Waliokuwa Ngariba katika wilaya ya Tarime mkoani Mara wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi ili wasirudie tena suala ukeketaji kwa watoto wa kike baada ya kupatiwa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji.

Awali Ngariba hao walidai kuwa kipindi cha ukeketaji hupata pesa nyingi jambo ambalo huwa ngumu kuacha kitendo hicho licha ya mashirika mbalimbali likiwemo shirika la AFGM Masanga kuendelea kutoa elimu juu ya madhara ya ukeketaji ili jamii iweze kubadilika.

Kwa kuliona hilo, shirika la ATFGM Masanga ambao ni wadau wa kupinga ukatili katika jamii waliamua kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa waliokuwa Ngariba lakini kwa sasa ili waweze kufanya kazi zinazotambulika na Serikali kwa lengo la kujipatia kipato na siyo kutegemea tena Ukeketaji.

Pia mafunzo hayo yamewashirikisha mabinti ili kuwajengea uwezo ili kuendelea kutoa elimu hiyo katika jamii inayowazunguka.

“Sisi kipindi cha ukeketaji tulikuwa tunapata pesa Nyingi lakini kwa sasa wazee wamekataa hatutakeketa tena hivyo tunaomba Serikali itupatie mitaji baada ya mafunzo haya tuliyoyapata”Aalisema Mmoja wa waliokuwa Ngariba wilayani Tarime

Akifunga mafunzo hayo, Katibu wa afya wilaya ya Tarime Neema Alphonce aliwataka waliokuwa Ngariba  pamoja na mabinti  hao kuendelea  kuwa mabalozi  wazuri katika jamii inayowazunguka huku wakitumia vizuri vikundi vilivyoundwa na kupewa elimu ya ujasiriamali.

Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo Stella Tungalaza alizidi kusisitiza kuzingatia vyema kile walichofundishwa darasani kwa lengo la kujikomboa na kuongeza Uchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la ATFGM Masanga , Sister Stella Mgaya alisisitiza wazee wa kimila kusimia vyema kauli ya kuwa mwaka huu hapatakuwa na ukeketaji na kuomba Serikali kuendelea kushirikiana vyema na mashirika hayo ili kuchukua hatua kali kwa wale watakaojihusisha na suala la ukeketaji.

“Wazee walishatoa kauli kuwa hakuna ukeketaji lakini wakurya wana tabia ya kujaribu hivyo wanaweza kujaribu kukeketa na Serikali isipofuatilia wanaongeza kasi ya kukeketa sasa tushirikiane zaidi ili kuondoa kabisa ukeketaji”. Alisema Mgaya.

Mkurugenzi wa Shirika la ATFGM Masanga Sister Stella Mgaya akizungumza kwenye mafunzo hayo

Recommended for you