Habari Picha

Parokia Mpya ya Mtakatifu Bikira Maria Buswel Jijini Mwanza Yazinduliwa

on

Judith Ferdinand,Mwanza

Waumini wa Parokia Mpya ya Mt.Bikira Maria Buswelu,iliyopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza, wametakiwa kuwa wamoja pamoja na kudumisha imani ya kikristu.

Wito huo umetolewa na Mhashamu Askofu Mkuu wa  Jimbo Kuu la Mwanza Jude Thaddeus Ruwa’ ichi wakati akizindua Parokia hiyo jana jijini hapa.

Askofu Ruwa’ichi alisema,waumini wa parokia hiyo wanatakiwa kudumisha imani ya kikristu kwa kurithisha imani hiyo kwa watoto na vijana,ili waweze kufanya kazi ya utume ngazi ya familia, jumuiya  ndogo ndogo,parokia mpaka jimbo.

Alisema,wanatakiwa kuwa na ushirikiano na parokia jirani sambamba na kuwa mstari wa mbele kuhakikisha ndani ya jamii haki na amani vinakuepo na utunzaji wa mazingira pia.

Pia alisema, wanatakiwa kulinda rasilimali za kanisa pamoja na  kuhimiza jamii kuishi kwa uadilifu, hivyo alimteua  Padre Francis Kwanga kuwa Paroko wa kwanza wa parokia hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Angeline Mabula alisema, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kutujalia uhai na kuweza kushuhudia uzinduzi wa parokia hiyo,kwani wengine hawakupata nafasi hiyo kwa vile wametangulia mbele ya haki.

Mabula aliwaomba,waumuni wa kanisa hilo kuendelea kumuombea Rais,viongozi pamoja na taifa,ili shughuli za uchumi ziweze kusonga mbele.

Pia alisema,waumini wa kikristu(Romani Katoliki) na   madhehebu mengine,wanatakiwa kuwa waadilifu katika imani zao, kufuata sheria pamoja na katiba,huku kila mmoja akitimiza wajibu wake ili kufikia uchumi wa viwanda.

Aidha alisema, wanatakiwa kuwa na mshikamano katika kujenga taifa,na ya kaisali mpe kaisali  hivyo wanatakiwa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi na kufikia uchumi wa kati.

Naye Katibu wa Parokia hiyo Sylivester Kwangulo alisema, changamoto inayowakabili ni waumini wa parokia hiyo kutoshiriki katika jumuiya ndogondogo pamoja na kutotii sheria  ya  kanisa Katoliki ya ndoa.

Vilevile Makamu Mwenyekiti Halmashauri Walei wa Parokia hiyo Julius Sabule alisema, parokia hiyo ilianza kama kigango mwaka 1918 huku waumini wakisali chini ya mti,ambapo  oktoba 22,2017 Askofu Ruwa’ichi  alitangaza kuwa ifikapo januari 1,2018 itakuwa parokia kamili na leo (jana),  katika kusherekea siku kuu ya mwaka mpya  ndio ameizindua rasmi.

Recommended for you