Habari Picha

POLISI MKOANI MWANZA WAINGIA LAWAMANI

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limeingia lawamani baada ya askari wake wanne wanaodaiwa walikuwa wamelewa kumfyatulia risasi mke wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Mapya, Kata ya Mabatini Jijini Mwanza, Editha Lucas (36) na kumjeruhi mguu wa kulia.

Katika tukio hilo, pia wananchi wengine walijeruhiwa kwa kipigo ambao ni pamoja na Mwenyekiti wa Mtaa  huo, Boniphace Ntobi (45), James Chacha (31), Lule Boniphace (41)  na aliyetambulika kwa jina moja la Hassan wote wakazi wa Mabatini.

Tukio hilo lilitokea juzi Agosti 8 majira ya saa nne usiku ambapo inadaiwa askari hao waliitwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo baada ya kutokea tukio la ajali ya daladala aina ya Toyata Hiace lenye namba za usajili T.394 DJW lililokuwa likiendeshwa na Amin Shaban (28) kugonga ukuta wa nyumba yake, lakini askari hao walipofika eneo hilo walianza kutoa vipigo kwa raia.

Mwenyekiti wa mtaa huo alisimulia kwamba mnamo saa nne za usiku baada ya  dereva wa daladala kugonga nyumba yake wakati akigeuza gari aliamua kupiga simu kituo cha polisi Mabatini kuomba askari wa usalama barabarani kufika, kushuhudia na kisha kuchukua taarifa za ajali hiyo lakini walipofika mambo yakaanza kwenda tofauti.

“Askari hao walikuja eneo la tukio  dakika 45  baada ya kupiga simu wakiwa wametanguliwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mabatini (OCS), walipofika niliwaonyesha dereva ambaye nilikuwa nimemshikilia baada ya wao kuniuliza dereva yuko wapi cha kushangaza walimvamia  mjumbe wa serikali ya Mtaa aliyekuwa amesimama karibu na dereva na kuanza kumpiga nikawaambia huyo siyo mtuhumiwa, nikawaonyesha dereva.

“Niliposema hivyo ndipo wakanigeukia mimi na kuanza kunipiga kwa kutumia kitako cha bunduki huku wengine wakinishambulia kwa ngumi, OCS akawaambia mnafanya nini huyo ni kiongozi wa serikali ya mtaa mbona hamnisikilizi ninavyowaambia…nikakimbilia ndani kwangu wakanifuata huko wakatuunganisha mimi na mke wangu wakatupiga na kutubamiza ukutani wakaanza kufyatua risasi hewani kitendo hicho kilisababisha  watoto kupiga kelele  kutokana na  taharuki hiyo na baada ya  kumpiga mke wangu waliondoka naye  usiku huo kwenda naye kituo cha Polisi,” Alisumlia Mwenyekiti.

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kesho yake asubuhi (jumatano) alienda kituoni alikopelekwa mke wake na kumchukua kumpeleka hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekoutoure lakini madaktari wakashauri apelekwe hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa kufanyiwa uchunguzi zaidi ili kubaini kama jeraha hilo linatokana na kupigwa risasi au ni jeraha la kitu kingine.

Naye mmoja wa wanafamilia, Amos Ntobi aliyeshuhudia tukio hilo alisema baada ya askari hao kufika eneo hilo Shemeji yake (Editha) alitolewa nje akiwa mtupu,  katika eneo hilo zinakadiliwa risasi takribani 15 zikipigwa hewani na kuzua taharuki kwa wananchi ambapo maganda ya risasi 14 yaliokotwa.

“Eneo la tukio  niliokota maganda ya risasi 14 na risasi moja ambayo haijatumika,   inasikitisha kuona tupo katika nchi ya amani lakini  polisi wanakikuka maadili ya kazi kwa kufanya vitendo vya  unyama kiasi hiki…. shemeji yangu ambaye ni mke wa  mwenyekiti wa Mtaa alipatwa na risasi  kwenye mguu wa kulia hadi hivi sasa yupo katika hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji mdogo,”Alisema mwanafamilia huyo.

Diwani wa Kata ya Mabatini, Deus Mbehe, alisema baada ya tafrani hiyo wananchi walipata taharuki na wengine kukimbia ovyo kutoka na kupata hofu ya milio ya risasi kwa kujua kuwa mtaa huo umevamiwa na waharifu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi jana alisema jeshi hilo linawashikilia askari wanne kwa mahojiano na endapo itathibitika walitumia nguvu kubwa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.

“Jeshi la polisi hatujawatuma kwenda kutumia nguvu mahali ambapo palihitaji majadiliano, uzuri ni kwamba mkuu wa kituo cha polisi alikuwepo wakati askari hawa wakitekeleza tukio kwa hiyo tunaamini kwamba uchunguzi wetu utakuwa wa haki na hautaegemea upande wowote. Alisema Msangi.

Recommended for you