Audio & Video

Shirika la Railway Children Africa lataka ushirikiano zaidi kutoka Serikarini

on

Judith Ferdinand, BMG

Serikali imehimizwa kuendelea kuwashirikisha kwa ukaribu zaidi wadau mbalimbali katika mipango na mikakati ikiwemo kutenga bajeti ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu (watoto wanaoishi mitaani).

Meneja Mradi wa Shirika la Railway Children Africa nchini Tanzania, Abdallah Issa ameyasema hayo wakati akizungumza na BMG katika ofisini za shirika hilo zilizopo Isamilo Jijini Mwanza na kubainisha kwamba ili kumaliza au kupunguza changamoto ya watoto wanaoishi mitaani, ni vema serikali ikashirikiana na wadau mbalimbali kwani pekee yake haiwezi.

Issa alisema serikali inatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya watoto hao ili iweze kushughulikia changamoto zilizosababisha wakakimbilia mtaani kwa urahisi pamoja kuhakikisha wanarudishwa makwao.

Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, jamii inatakiwa kuwa na  mtazamo chanya juu ya watoto wanaoishi mitaani kwani mtaa hauzai mtoto hivyo wawe na msimamo utakaosaidia kupunguza au kumaliza watoto wanaoishi mitaani.

Alibainisha kwamba shirika ambalo linatetea watoto wanaoishi mitaani, lengo lake ni kuona linapunguza au kutokuwa na watoto wa mitaani kwa kuwa na miradi mingi pamoja na kufanya kazi na mashirika mengi zaidi ili kuweza kufikia watoto wengi zaidi nchini.

“Katika kuendeleza juhudi za kumaliza changamoto hiyo, tulianzisha mradi unaoitwa Jamii Inayojali (Community Care) ambapo tunawashirikisha wanajamii wakiwemo madereva, wapiga debe, makondakta na mama ntilie ili wanapowaona watoto wageni katika maeneo yao wafanye taratibu za kuwarudisha makwao au kutoa taarika ngazi husika ikiwemo katika shirika letu”. Alisema Issa.

Vile vile alisema shirika kupitia mradi wake wa Kivuko wa miaka miwili unaotarajia kuisha June mwaka huu, wamefanikiwa kuwarudisha watoto 79 makwao na kuwapatia vifaa vya shule pamoja na familia zao ili kuwezeshwa kiuchumi kwa wanaohitaji kufanya biashara huku vijana 85 waliokuwa wanaishi mazingira magumu wamewezeshwa kufanya ujasiriamali.

Kadhalika alisema kupitia mradi huo, pia wamewezesha familia 33 katika kilimo na vijana 47 kwenye kilimo na ufugaji na wamewapa pesa kwa ajili ya kununua shamba na mahitaji mengine hivyo wanatoa semina kwa vijana ambao bado wana tabia mbaya ili waweze kubadilika.

Alisema baada ya kuanzishwa kwa mradi huo, familia na vijana wamepata mabadiliko kwani wamewezeshwa katika kilimo, biashara na ufugaji hatua itakayosaidia kujitegemea kiuchumi na kuajiri wengine na hivyo kusaidia kuondokana na wimbi la watoto wanaoishi mitaani.

Bonyeza HAPA kumbukumbu ya vijana waliouawa kikatili.

Recommended for you