Audio & Video

Sababu na Suluhisho la Watoto wanaoishi Mitaani

on

Baadhi ya watoto wanaoishi mtaani Jijini Mwanza ambao wanahudumiwa na shirika la Railway Children Afrika wakijifunza kusoma na kuandika.

Imeandaliwa na Judith Ferdinand

umekuwa na ongezeko la watoto wanaoishi mitaani Jijini Mwanza siku hadi siku la watoto licha ya Serikali, wadau, mashirika na asasi mbalimbali kufanya jitihada na kuweka mikakati ya kuhakikisha hakuna changamoto ya watoto wanaoishi mitaani.

Hata hivyo zipo sababu kadhaa zinazoelezwa kwamba ni kichocheo cha kusababisha ongezeko hilo. Mwaka jana kwenye uwanja wa Furahisha katika maadhimisho ya Siku ya Watoto Wanaoishi Mtaani Duniani inayoadhimishwa Aprili 12 kila mwaka, nilipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kueleza sababu za kukimbilia mtaani na hata changamoto wanazokumbana nazo.

Nilizungumza na mtoto Vumilia Mrasa ambaye ni miongoni mwa watoto wanaoishi mitaani Jijini Mwanza, alisema sababu kubwa inayosababisha kuwepo na ongezeko la watoto wa mitaani ni kutowajibika ipasavyo kwa wazazi katika makuzi na malezi ya watoto pamoja na kutowapatia mahitaji muhimu kama elimu, afya, chakula na malazi na hivyo kuamua kukimbilia mitaani.

Pia anasema sababu nyingine ni ugomvi wa wazazi kwenye familia, umasikini, vifo vya wazazi, ushawishi wa makundi rika, ugomvi wa kifamilia, tumaini la kuwa na maisha mazuri, utovu wa nidhamu pamoja na sababu za kidini na kimila.

Naye Kelvin Ramadhani anaeleza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakiwa mtaani kuwa ni  vifo, ukosefu wa chakula, malazi, mavazi, matibabu, kufanyiwa vitendo vibaya ikiwemo kunyanyaswa kingono na kijinsia, ukosefu wa haki ya kupendwa na kupatiwa elimu, kupigwa kama wezi, kukosa msaada kutokana na jamii kuwabagua na kuwaita majina mabaya kama chokoraa, watoto wa mbwa, kuingia kwenye makundi mabaya pamoja na kukosa haki ya malezi.

Hata hivyo anasema wao ndio wamekua waathirika wakuu endapo kunatokea magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu au hali yoyote ya hatari kutokana na mazingira wanaoishi kuwa hatarishi na kutopewa kipaumbele cha kupatiwa huduma muhimu na ulinzi.

Kwa upande wake Emmanuel John alitoa wito kwa serikali, jamii, mashirika na asasi mbalimbali kuwaongeza watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika vipaumbele vyao ikiwemo kuwalinda na kuwasikiliza.

“Sisi watoto tulio katika mazingira magumu tunaomba wadau kwa ujumla wenu muendelee kutusaidia kwa dhati, tuchukulieni kama ndugu na rafiki, tupendeni, mtuthamini, mtulinde, mtujali, tuleeni vyema na kutupatia elimu.” Anasema John.

Aidha aliwaomba wazazi na walezi kuhakikisha familia ni mahali salama pa kuishi pamoja na jamii, serikali na wadau wengine kuwajibika ipasavyo hatua ambayo itasaidia kumaliza changamoto au kupunguza ongezeko la watoto wanaoishi mitaani.

Nilitembelea shirika la kuhudumia watoto na vijana wanaoishi mtaani la Railway Children Afrika lililopo Isamilo Jijini Mwanza ambapo Meneja Msaidizi wa Mradi wa Kivuko kutoka  shirika hilo Mary Mushi naye alielezea sababu za ongezeko la watoto wa mitaani, changamoto, mikakati pamoja na ushauri kwa jamii na serikali.

Anasema suala la ukosefu wa malezi bora kwa watoto ni miongoni mwa sababu kikubwa zinazochochea ongezeko la watoto wanaoishi mitaani na kwamba wazazi wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi katika shughuli za kiuchumi na kusahau malezi ya watoto.

Anasema sababu nyingine ni mabadiliko ya utandawazi ambapo imepelekea migogoro baina ya watoto na wazazi ambao wanataka waishi kwa kufuata utaratibu wa kizamani hivyo wanaona wananyanyaswa na kutafuta njia mbadala ya kukimbilia mtaani ili wawe huru.

Hata hivyo anasema utoaji wa adhabu kali  na utumiaji wa silaha kwa watoto pale wanapokosea ni miongoni mwa sababu ya kukimbilia mtaani kutafuta msaada wakidhani ni sehemu salama.

Anasema jamii na wazazi kutofuata njia ya uzazi wa mpango pia ni sababu ya ongezeko hilo kutokana na kuzaa watoto wengi ambao wanashindwa kuwapatia mahitaji muhimu hivyo kuamua kukimbilia mtaani kuomba msaada kwa wasamaria wema.

Vilevile anasema sababu nyingine ni kutengana kwa wazazi, migogoro ya ndoa, umaskini pamoja na mmomonyoko wa maadili. Anasema njia itakayosaidia kupunguza au  kumaliza changamoto ya watoto wanaoishi mitaani ni wanafamilia kutumia njia za uzazi wa mpango (family plan) ili kupanga idadi ya watoto watakaoweza kuwahudumia kulingana na uwezo wao kiuchumi.

Vijana hasa wanafunzi wa vyuo wajikinge na mimba zisizotarajiwa na jamii ihakikishe inapinga ndoa za utotoni. Pia wazazi wajaribu kutenga muda wa kukaa na watoto wao, kuzungumza nao, kuwapenda, kuwasikiliza pamoja na kupunguza ukali ili kujua changamoto wanazokumbana nazo.

Aidha anaeleza kuwa familia moja inatakiwa kuwa na upendo na familia jirani na kuona watoto wote ni wao pamoja na kuwasaidia. Hata hivyo anasema licha ya serikali kuwa inawasaidia kwa namna moja ama nyingine, lakini inatakiwa iangalie jinsi gani familia na jamii inazifahamu sheria zinazomlinda mtoto.

Kadhalika amewataka viongozi wa serikali za mitaa kuangalia kwa ukaribu familia ambazo zipo katika mazingira magumu siyo tu kwa chakula bali pia kwenye suala la malezi.

Kadhalika anasema, watashirikiana na mama lishe, wapiga debe na makondakta na sehemu zote zinazoonekana kuwa kimbilio la watoto hao pale wanapotoka makwao ili waweze kuwasaidia na kuwarudisha majumbani kwao.

Mwenyekiti wa Mtaa wa  Nyamanoro Mashariki Trasisius Kabuche anasema ili kukomesha suala hilo jamii inapaswa kumrudia Mungu na kuwa na upendo pamoja na kuzingatia maadili na kila mmoja kuwajibika kwa nafasi yake.

Pia anasema jamii inatakiwa kuwasaidia kwa hali na mali wale walezi watakaojitoa kuwalea watoto ambao wamepoteza wazazi wao ili kuondoa tatizo hilo na kuacha kukaa katika vituo jambo linalowafanya wajione wametengwa na jamii.

Hata hivyo anasema kila kiongozi wa  mtaa anatakiwa kuwa na taarifa sahihi ya watoto ambao hawana wazazi na wanahitaji msaada ili kuhakikisha wanapunguza tatizo hilo ambalo linaanzia ngazi ya familia na mtaa sambamba na kuwajibika ipasavyo kwa kuhakikisha watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu wanarudishwa kwao.

Aidha anasema,serikali inatakiwa kuweka mikakati ya kudumu ambayo,haitampa nafasi mtoto kuja  kukaa mtaani na hapaone siyo sehemu salama kwa maisha yake.

Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Willbard Kilenzi anasema atakaa na baraza la madiwani kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuweka mikakati ya kuhakikisha tatizo la watoto wanaoishi mitaani linapungua au kumalizika kabisa.

Afisa Ustawi wa Jamii Sekretalieti ya Mkoa wa Mwanza, Wambura Kizito anasema kutokana  na changamoto ya ongezeko la watoto wanaoishi mitaani ambayo sababu kubwa ni watoto kukosa mahitaji muhimu katika familia, wazazi wanatakiwa kutumia njia ya uzazi wa mpango ili kupanga na kupata watoto watakaoweza kuwatimizia mahitaji muhimu kulingana na kipato chao.

“Jamii na wazazi wajitahidi kuwa na mikakati kabla ya kuwa na familia ili kujua wanataka watoto wangapi, wakati gani ambao wataweza kuwatimizia mahitaji muhimu kulingana na hali ya kipato chao kiuchumi, na waachane msemo wa kila mtoto na riziki yake kwani umepitwa na wakati”. Anasema Kizito.

Kizito anasema watoto wanapokosa mahitaji muhimu na malezi sahihi kutoka kwa wazazi wao ambao ndio nguzo, wanakimbilia mtaani kutafuta msaada kutoka kwa wasamaria wema,hivyo kujikuta wakiishia kuombaomba.

Anasema serikali wadau na mashirika mbalimbali wanatakiwa kuhakikisha wanatoa elimu ya malezi ambayo itasaidia wazazi kujitambua na kujua wajibu wao kwa watoto pamoja na wazazi kuhakikisha  migogoro ndani ya familia inatatuliwa  bila kumuathiri mtoto.

Pia anasema wanashirikiana na shirika la Railway Children Afrika kuwaunganisha watoto hao na familia na kuwarudisha shuleni na kuongeza kuwa kabla ya kuwarudisha nyumbani wanawaweka kwenye makao kwa muda kwa ajili ya kuwasiliana na familia zao na kuzitembelea hili kubaini changamoto zinazopelekea kukimbilia mtaani.

Vilevile akasema mikakati ya mkoa ni  kuhakikisha kila halmashauri kupitia maofisa ustawi wa jamii inatoa elimu ya kifamilia na malezi kuanzia ngazi ya Kata pamoja na kubaini changamoto zilizo sababisha mtoto kukimbilia mtaani ili kuboresha familia zao.

Aidha anasema kila halmashauri inatakiwa kutenga bajeti kuhusu makundi maalumu ikiwemo watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ikiwa ni mkakati wa serikali kuwasaidia watoto hao waweze kurudi makwao ili kuepukana na kupunguza changamoto hiyo kwani wakiachwa kutakua na mkoa na taifa la watoto wanaoishi mitaani, kutokana na  mabadiliko ya kimwili wataendelea kuzaliana na hivyo  kuwa na wajukuu wanaoishi kwenye mazingira hatarishi zaidi.

Kadhalika anasema halmashauri zote zinapaswa kuweka utaratibu wa kuzungumzia masuala ya ustawi wa jamii ikiwemo suala la watoto wanaoishi mitaani kupitia vyombo vya habari ili kutoa elimu kwa jamii.

Pamoja na hayo anawaomba wanasiasa kuimarisha uchumi wa nchi na wanapokuwa wanazungumza na wananchi kwenye majukwaa, wazungumzie pia masuala ya ukatili na kuwashauri wananchi kutumia njia za uzazi wa mpango.

Imehaririwa na George Binagi

Recommended for you