Habari Picha

SAMAKI ZIWA VICTORIA HATARINI KUTOWEKA, WAZIRI WA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI AMUNG’UNYA MANENO KWA WAMILIKI WA VIWANDA VYA SAMAKI MKOANI MWANZA.

on

Dk.Titus Kamani

Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk.Tutus Kamani amebainisha kwamba Mazao ya
Samaki ndani ya Ziwa Victoria yameanza kupungua, kutokana na Uvuvi haramu na
hivyo kuhatarisha Uchumi wa Taifa sanjari na kupunguza upatikanaji wa ajira kwa
Wananchi.

Dk.Kamani ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Busega Mkoani Simiyu aliyasema
hayo jana Mkoani Mwanza, wakati akizungumza katika kikao na wamiliki wa Viwanda
vya Samaki Mkoani Mwanza, kikao ambacho kililenga katika kujadili na kupeana
taarifa ya nini kifanyike ili kuboresha Sekta ya Uvuvi hapa nchini.
Katika kikao hicho Dk.Kamani alieleza kwamba katika Ziwa Victoria
zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uvuvi ikiwemo kupungua kwa
mapato kutokana na Mazao ya Samaki kupungua ziwani, jambo ambalo linatokana na
ongezeko la wavuvi wanaovua bila kuwa na mpangilio mzuri wa Uvuvi endelevu
sanjari na Uwepo wa Uvuvi haramu katika Ziwa hilo.
“Uvuvi ya zana haramu kwa maana ya uvuvi haramu unaathiri kiwango
cha Samaki na mimi mwenyewe nimeshuhudia, tulienda na watu wa TAFIRI (Tanzania Fisheries Research Institute) tukaingia ziwani wakatumia
utalaamu wao kwa muda wa nusu saa hatukupata hata samaki mmoja mwenye sifa ya
kwenda kiwandani na hiyo ilikuwa ni ishara kwamba kuna tatizo”.Alisema
Dk.Kamani huku akiongeza kuwa japo hiyo haitoshi kisayansi kutoa hitimisho
kwamba hakuna samaki ziwa Victoria.
Dk.Kamani akizungumza na wanahabari
Huku akishindwa kutaja majina, Dk.Kamani alibainisha
kwamba Suala la Uvuvi haramu linajumuisha watu wengi ambao ni pamoja na
wananchi wenyewe, watendaji wa Serikali sanjari na baadhi ya Wamiliki wa
Viwanda vya kuchakata Mazao ya Samaki, hali ambayo ameonya kuwa inaweza
kuhatarisha uchumi wa Taifa pamoja na Upatikanaji wa ajira ambapo amebainisha
kuwa muda si mrefu kila mmoja ataathirika kutokana na suala la uvuvi haramu na
hivyo kuomba ushirikiano ili kutokomeza hali hiyo.

Katika hatua nyingine Dk.Kamani aliwasihi
wamiliki wa viwanda kutojiingiza katika suala la kununua samaki wachanga kwa
kuwa kuna baadhi ya taarifa kwamba baadhi ya viwanda vinajihusisha na ununuzi
wa samaki wachanga (wanaovuliwa kwa njia haramu) jambo ambalo linahatarisha
upatikanaji wa samaki katika Ziwa Victoria.
Ili kuboresha Sekta ya Uvuvi hapa nchini,
Dk.Kamani alibainisha kwamba Serikali imeandaa Mkakati katika bajeti ijayo kwa
ajili ya kupata fedha ambazo zitasaidia katika kuinua sekta ya Uvuvi hapa
nchini, huku akitoa rai kwamba suala la kupambana na Uvuvi haramu katika ziwa
Victoria lisiingiliwe na itikadi za kisiasa pale watendaji wa sekta ya uvuvi
wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Dk.Kamani na Wanahabari katika Mahojiano.
 Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mh.Baraka Konisaga aliahidi kushirikiana na
wamiliki wa viwanda vya kuchakata Samaki Mkoani Mwanza, Sanjari na Wavuvi
wenyewe kwa lengo la kuboresha Sekta hiyo ya Uvuvi Mkoani Mwanza.

‘Nitatumia ushawishi wangu pindi Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo ambae yuko nje ya nchi kwa shughuli za
kiofisi, atakaporejea katika majukumu yake ili aweze kukutana na wavuvi pamoja
na wamiliki wa viwanda vya samaki Mkoani Mwanza ili kujadili nini cha kufanya
ili kuboresha sekta hii”. Alisema Konisaga huku akionyesha tabasamu kama ilivyo
kawaida ya kiongozi huyo ambae anafahamika kwa jina la Mtumishi wa Mungu.
Dk.Kamani
Akitoa Mchango wake kama miongoni mwa wamiliki
wa Viwanda Mkoani Mwanza ambao wamekutana na Dk.Kamani ambae ni Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,  Murtaza
Alloo ambae ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VicFish alieleza kwamba viwanda vikubwa
havijishughulishi na ununuzi wa samaki wachanga (wanaovuliwa kwa njia haramu),
badala yake suala hilo hufanywa na baadhi ya viwanda vidogo vidogo vyenye
leseni na hivyo kuomba Serikali kuvichukulia hatua viwanda hivyo.

Aidha alimtaka Waziri Kamani kubainisha
viwanda ambavyo anadhani vinanunua samaki ambao ni wachanga, (wanaovuliwa kwa
njia haramu), jambo ambalo Dk.Kamani amebainisha kwamba si vyema kuliweka
hadharani na hivyo kuvionya viwanda hivyo kwa kuvitaka kuachana na tabia hiyo
la sivyo vitachukuliwa hatua kali za kisheria.
Takribani wamiliki na wawakilishi wa Viwanda
vinane vya Kuchakata mazao ya Samaki Mkoani Mwanza waliweza kujumuika kwa
pamoja na Dk.Kamanin katika kikao hicho, ambapo suala kubwa lililosisitizwa ni
juu ya kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha kuwa anaisaidia Serikali katika
kutokomeza uvuvi haramu ili kuwa na uvuvi endelevu hapa nchini, huku wamiliki
hao wakisisitizwa zaidi kutonunua mazao ya samaki yaliyovuliwa kwa njia haramu.
Viwanda hivyo ni Nile Perch Feshers, Kagera
Fish, Omega Fish, Tz Fish & Musoma Fish, VicFish na Victoria Fish ambapo
mara baada ya Dk.Kamani kuzungumza na wawakilishi na wamiliki hao wa Viwanda,
pia alipata fursa ya Kuzungumza na baadhi ya wavuvi na viongozi wao Mkoani
Mwanza.