Audio & Video

Serikali yasisitiza sheria ya chakula, dawa na vipodozi itumike ipasavyo

on

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TFDA, Bi. Agnes Kijo (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo, Bi.Zamarad Kawawa (kulia) wakiwa kwenye kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Judith Ferdinand, BMG

Imeelezwa kuwa afya ya watumiaji bidhaa mbalimbali zitalindwa na kuboreshwa ikiwa sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura 219 itasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo huku vyombo vya habari vikitimiza wajibu wake kwa usahihi.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, Bi.Zamaradi Kawawa aliyasema wiki hii Jijini Mwanza katika kikao kazi  cha Wahariri na Waandishi wa Habari kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga kuhusu uhamasishaji wa sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura ya 219 kilichoandaliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA).

Kawawa alisema wahariri na waandishi wa habari wanamchango mkubwa katika kuhimiza utekelezaji  wa sheria hiyo, kuelimisha umma kwa kuwapatia taarifa sahihi zinazohusu shughuli za udhibiti wa  bidhaa hizo kutoka vyanzo mbalimbali sambamba na kuijua sheria hiyo.

Alisema vyombo vya habari vinawajibu wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii kuhusu udhibiti wa bidhaa, kuielimisha juu ya kuzingatia ubora na usalama wa bidhaa hizo pamoja na kuwaibua watu wanaovunja sheria hiyo kwa kutoa taarifa TFDA na kwa vyombo vingine vya sheria vinavyohusika na udhibiti.

Aliwahimiza wanahabari kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara watakayo yapata kiafya endapo watatumia bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi ambayo vipo kinyume na sheria na kutoa mapendekezo  kwa TFDA juu ya namna ya kuboresha usimamizi na utekelezaji wa sheria.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TFDA, Bi.Agnes Kijo alisema suala la afya ni la jamii nzima hivyo ni wajibu wakila mtu katika kudhibiti bidhaa bandia na duni huku waandishi wakiendeleza ushirikiano na mamlaka hiyo kuwafichua wafanyabiashara wasiowaaminifu wanaouza bidhaa zilizopita muda.

Kijo alisema kwa mwaka wanatumia zaidi ya shilingi milioni 100 katika kufanya oparesheni na ukaguzi maalum wa kudhibiti bidhaa hizo hivyo ni vyema wananchi wakahamasishwa na kuelimishwa ili kuachana na matumizi ya bidhaa zenye viambato sumu hatua itakayosaidia kutumia fedha hizo katika miradi ya maendeleo.

Naye Mwanasheria Mshauri wa TFDA, Iskari Fute alisema madhumuni ya sheria ni kuweka mfumo thabiti wa usalama, ubora na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba, vitendanishi, vifaa vya maabara na dawa zenye asili ya miti shamba pamoja na kulinda afya ya jamii ili kutekeleza msingi wa haki ya kuishi.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Dawa na Bidhaa Nyongeza wa TFDA, Adam Fimbo alisema bidhaa wanazodhibiti ni zile zenye athari moja kwa moja katika afya ya mtumiaji hivyo waandishi wa habari wana mchango mkubwa wa kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya bidhaa hizo.

Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho waliitaka mamlaka hiyo kufika hadi maeneo ya vijijini kutoa elimu kuhusu madhara yatokanayo na utumiaji wa vipodozi vyenye viambato sumu, bandia na duni.

ISOME PIA HABARI HII Wanahabari mikoa ya Mwanza na Shinyanga wapewa semina na TFDA 

Recommended for you